Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akmikabidhiwa nyaraka za makabidhiano ya ofisi na aliyekuwa Waziri wa Ardhi William Lukuvi katika hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi iliyofanyika ofisi ya Wizara iliyopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza wakati wa makabidhiano ya ofisi baina yake na aliyekuwa Waziri wa Ardhi William Lukuvi katika hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi iliyofanyika ofisi ya Wizara iliyopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
akiagana na aliyekuwa Waziri wizara hiyo ambaye ni Mbunge wa jimbo la Isimani
William Lukuvi wakati wa makabidhiano ya ofisi yaliyofanyika ofisi za Wizara
zilizopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dar es Salaam.
................................
Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Aliyekuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi
amemkabidhi Ofisi aliyekuwa Naibu wake Dkt Angeline Mabula ambaye sasa ni Waziri
wa Wizara hiyo.
Makabidhiano ya ofisi yamefanyika leo tarehe 17 Februari 2022 kwenye
ofisi za Wizara hiyo katika mji wa serikali Mtumba jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Lukuvi alisema ana furaha kubwa
kumkabidhi ofisi mtu anayeijua Wizara na aliyekuwa akifanya kazi naye.
‘’ Dkt Angela anayajua mengi kwenye wizara, tumeshirikiana katika
kushughulukia dhuluma na malalamiko ya ardhi na katika kipindi chote
tumejitahidi kupunguza malalamiko na yamepungua’’. Alisema Mbunge wa jimbo la
Isimani
‘’Ninaomba mumpe ushirikiano, nimefanya naye kazi takriban miaka sita na
tumeelewana sana na nilimpa kazi nyingi kwa sababu ana uwezo, tofauti yangu
mimi na yeye ni kuwa, mimi ni mkali ila yeye ni mpole’’ alisema Lukuvi
Kwa mujibu wa Lukuvi, wakati wa uongozi wao, Wizara ya Ardhi ilipiga
hatua kubwa katika masuala mbalimbali yakiwemo mabadiliko ya mfumo wa utunzaji
kumbukumbu za ardhi sambamba na uanzishwaji ofisi za ardhi za mikoa.
Ameishukuru Menejiment ya Wizara kwa kuonesha ushirikiano wakati wa
kipindi chote alichokuwa Wizara ya Ardhi na kuitaka menejiment hiyo kumpa
ushirikiano Waziri wa sasa Dkt Mabula.
Kwa upande wake Dkt Mabula mbali na kumpongeza mhe Samia Suluhu Hassan,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumuamini na kumteua kuwa Waziri wa
Ardhi alimshukuru Lukuvi kwa kumpa uhuru wa kufanya kazi wakati wote
alipokuwa wakifanya kazi pamoja.
Alisema, katika kipindi cha uongozi wao, wizara ya ardhi imefanya mambo
mengi kwa lengo la kuondoa changamoto za sekta ya ardhi na kubainisha kuwa
mafanikio yote yalitokana na ushirikiano na menejiment ya wizara.
‘’Mengi yamefanyika kuondoa changamoto kwa ushirikiano na timu nzima ya
Menejiment, umenilea vizuri, malezi na imani uliyokuwa nayo ni wazi nina deni
kubwa la kulipa katika utendaji kazi’’
Waziri Dkt Mabula aliongeza kuwa, pamoja na mambo mengine lakini
msisitizo wa wizara yake kwa sasa mbali na mambo mengine ni vipaumbele vya rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika masuala ya
uwekezaji na mifumo ya utunzaji kumbukumbu za ardhi.
Aliyekuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye ni Mbunge wa jimbo la Isimani mkoani Iringa William Lukuvi aliondolewa nafasi ya uwaziri katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanyika mapema januari mwaka huu. Lukuvi aliteuliwa kwa mara ya kwanza nafasi ya uwaziri mwaka 1995 katika iliyokuwa wizara ya kazi na baadaye kuhudumu Ofisi ya Waziri Mkuu na baadaye Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambako alidumu kwa miaka 8 tangu mwaka 2014.
Post a Comment