TFRA YAFIKIA ASILIMIA 93 UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YAKE





...........................................

Imeelezwa kwamba Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imefikia asilimia 93 ya utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hiyo kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Julai mpaka Desemba 2021 kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Hayo ni mafanikio makubwa kwa taasisi ambapo bado imeweka mikakati na malengo ya kuhakikisha inatekeleza majukumu yake kwa asilimia mia moja.

Hayo yamebainishwa tarehe 11 Februari, 2022 na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo, Dkt. Stephan Ngailo alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi kwa kipindi cha tajwa kwa watumishi wa TFRA katika kikao cha kawaida cha wafanyakazi kinachofanyika kila robo ya muhula ya mwaka wa fedha.

Pamoja na kueleza mafanikio hayo, Dkt. Ngailo amewapongeza watumishi wa Mamlaka hiyo kwa mchango wao katika kufikia mafanikio hayo na kuwataka kuimarisha mawasiliano na mahusiano miongoni mwao ili kuboresha utendaji na kuifanya Mamlaka ifikie malengo iliyojiwekea.

“Kila mmoja ana mchango wa kumfanya mwingine atekeleze majukumu yake hivyo tufanye kazi kwa kutegemeana na tupafanye mahala pa kazi kuwa ni mahala salama na mahala pa kupafurahia” Dkt. Ngailo alisisitiza.

Akikazia kuhusu suala la udhibiti ubora wa mbolea  ikiwa ni jukumu mama la Mamlaka hiyo, Dkt. Ngailo amewataka maafisa udhibiti kuhakikisha wanaimarisha shughuli za udhibiti wa mbolea katika maeneo yao ya kazi na kuhakikisha mbolea inayoingia na kutoka nchini inakidhi viwango vya ubora vinavyokubalika na hivyo kuleta matokeo chanya kwa wakulima nchini.

Aidha, Dkt. Ngailo amewataka watumishi wa Mamlaka hiyo kutokujihusisha na masuala ya ulevi wakati wa kazi na kusisitiza suala la ulevi kazini halikubaliki.  “Niwaombe sana mameneja wa kanda mzingatie suala la maadili kazini hasa ulevi wakati wa kazi, nizamu ni lazima” Dkt. Ngailo alisisitiza.

Mwisho Dkt. Ngailo amewataka mameneja wa kanda kuwa na mahusiano mazuri na viongozi wa mikoa na wilaya katika kanda wanazozisimamia. “Mwende mkashirikiane kikamilifu na wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, watendaji wote katika ngazi za mikoa na wilaya pamoja na wadau wote wa sekta ikiwemo wakulima, wazalishaji na wafanyabiashara wa mbolea” Dkt. Ngailo alikazia.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi, Victoria Elangwa amesema Mamlaka ipo katika hatua nzuri ya utekelezaji wa majukumu lakini inaendelea kuboresha mpango mkakati wake ili uendane na mpango mkakati wa Taifa na hivyo kugusa kikamilifu agenda za kitaifa katika kuwaletea maendeleo watanzania.

Akitoa taarifa ya kikao cha bodi ya wakurugenzi ya Mamlaka hiyo kwa watumishi wake, Elangwa amesema Bodi imeridhishwa na utendaji wa Mamlaka kutokana na kusimamia na kutekeleza majukumu kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali inayosimamia Mamlaka hiyo.

Pamoja na hayo, Elangwa amewasihi watumishi hao, kubuni mbinu za kuongeza vyanzo vya mapato vya taasisi  huku kila mmoja akiendelea kuboresha utendaji katika eneo lake la kazi.

Kikao hiki ni cha pili kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 ambapo Mamlaka imejiwekea utaratibu wa kufanya vikao kila robo ya Mwaka ili kujifanyia tathmini ya utendaji wa kila siku wa Mamlaka na kurekebisha kasoro zinazojitokeza na kukwamisha utendaji.



0/Post a Comment/Comments