Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akizungumza na wanahabari jijini Dar es salaam Katika kuadhimisha siku ya Hali ya Hewa Duniani
Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA) akizungumza na wanahabari jijini Dar es salaam Katika kuadhimisha siku ya Hali ya Hewa Duniani.
..........................
NA MUSSA KHALID
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amewataka wananchi na wadau mbalimbali, kuchukua tahadhari na kufuatilia taarifa za hali ya hewa, zinazotolewa na Mamlaka za Hali ya Hewa nchini (TMA) pamoja na kutekeleza maelekezo yanayotolewa.
Profesa Mbarawa ametoa kauli hiyo leo Jijini Dar es salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kuadhimisha siku ya hali ya hewa Duniani, kama sehemu ya kumbukumbu ya kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani tangu Machi 23, 1950.
Profesa Mbarawa amesema, Nchi zenye kipato cha chini na kati zinakabiliwa na changamoto kadhaa katika upande wa sekta ya hali ya hewa kutokana na uwezo mdogo wa matumizi sahihi ya taarifa kwa wananchi.
‘Ingawa kuna juhudi kubwa za Serikali za nchi mbalimbali na wadau katika kuboresha taarifa za tahadhari dhidi ya majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa na kusababisha maafa bado changamoto ni kubwa hususan katika nchi za kipato cha chini na cha kati ikiwa ni pamoja na Tanzania’amesema Profesa Mbarawa
Aidha amesema katika kukabiliana na maafa yanayoendelea kutokea, na kwa mtazamo kwamba hali ya hewa haitambui mipaka ya kijiografia, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikifanya jitihada za kushirikiana na washirika na wadau mbalimbali katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa katika utekelezaji wa sera zenye lengo la kukabiliana na kupunguza athari za maafa, programu na mipango ya kupunguza athari za majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa.
“Katika kuadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani mwaka huu, ningependa kutoa wito kwa watumiaji na wadau wote wa taarifa na huduma za hali ya hewa, hususan jamii inayoathirika zaidi na sekta zote za kijamii na kiuchumi kuchukua juhudi za makusudi kufuatilia taarifa na tahadhari za hali ya hewa
zinazotolewa na TMA. Nawahimiza mzitumie vyema taarifa hizi kwa ajili ya kupanga vyema shughuli zenu mbalimbali za maendeleo na katika kufanya maamuzi sahihi kwa ustawi na maendeleo endelevu ya nchi yetu”ameendelea kusisitiza Prof Mbarawa
Dkt. Agnes Kijazi ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) amesema, TMA imejipanga kuhakikisha inafuatilia mifumo ya hali ya hewa pamoja na kuwa na njia nzuri ya kuhakikisha taarifa sahihi zinawafikia wananchi mapema na hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
Dkt Kijazi amesema kuwa katika kuhakikisha majanga yanafuatiliwa na kutolewa tahadhari kwa wakati kwa jamii, wadau na wafanya maamuzi nchini, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imekuwa ikitoa tahadhari kupitia vyombo vya habari na njia zingine ikiwemo mitandao ya kijamii ili kuhakikisha kuwa taarifa za hali mbaya ya hewa zinawafikia walengwa kwa wakati
“Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kama Taasisi yenye dhamana ya utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini imeendelea kuongeza uwezo wa kutoa huduma za uhakika na kwa wakati za kila siku, siku tano, siku kumi, mwezi na msimu kwa watumiaji mbalimbali ikiwemo jamii, taasisi za umma, taasisi binafsi, mashirika, watunga na wasimizi wa sera. Katika kufanikisha hilo Mamlaka imeanzisha dawati maalumu ambalo linajukumu la kuandaa na kutoa utabiri mahususi wa kisekta kulingana na matakwa ya watumiaji’amesema Dkt Kijazi
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi jijini la Dar es salaam wameiomba Mamlaka ya Hali ya Hewa kuendelea kutoa elimu ya masuala ya hali ya hewa mara kwa mara kutokana na baadhi ya wananchi kutokuwa na ufahamu wa masuala ya hali ya hewa.
Maadhimisho ya mwaka huu yamekwenda sambamba na kauli mbiu isemayo ‘Tahadhari kwa Hatua za mapema’hivyo jamii imeendelea kusisitizwa kuzitumia taarifa zinazotolewa na mamlaka ya hali hewa ili kupunguza madhara yanayotokana na hali mbaya ya hewa.


Post a Comment