MEYA wa Manispaa ya Kigamboni Ernest Mafimbo amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha uzinduzi wa filamu ya 'Royal Tour' na kusisitiza kuwa itazidi kulitangaza Taifa la Tanzania Duniani
Akizungumza Dar es Salaam saa chache tangu kuzinduliwa rasmi kwa filamu hiyo katika Jiji la New York nchini Marekani, Mafimbo alisema kwa kufanikisha hatua hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan anazidi kuonyesha kwa vitendo dhamira yake ya kuiletea maendeleo Tanzania.
" Nichukue fursa hii kumpongeza Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ukweli anazidi kufanya mambo makubwa kwa Taifa hili kwa kipindi kifupi tangu aingie madarakani, Mungu aendelee kumlinda na kumsimamia " alisema Mafimbo
Alisema kuzinduliwa kwa filamu hiyo inayoonyesha vivutio mbalimbali vya utalii na kitamaduni, kutazidi kuongeza idadi kubwa ya watalii wanaoingia nchini kwa lengo la kuja kuvitazama hatua ambayo itasaidia kukuza pato la Taifa kutokana na fedha za kigeni.
Aidha Mafimbo amewataka watanzania wote kwa umoja wao kuendelea kumuunga mkono Rais Samia ili aweze kutimiza malengo yake ya kuiletea nchi maendeleo jambo ambalo pia litawezesha kuongezeka kwa kipato cha mtu mmoja mmoja.
Awali mapema usiku wa kuamkia leo, Rais Samia Suluhu Hassan alishiriki uzinduzi wa filamu hiyo ya Royal Tour aliyoshiriki kuicheza, uzinduzi ambao ulioudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo mashuhuri.
Saa chache kabla ya uzinduzi huo, Rais Samia alishiriki mkutano na baadhi ya watu maarufu uliofanyika kwenye klabu ya faragha ya Lotos hapa New York, na miongoni mwa waliohudhuria ni Meya mashuhuri wa jiji la New York, Eric Adams, ambaye ameeleza kuipenda Tanzania na kuahidi kuitangaza zaidi katika jiji lake la New York.
Mtu mwingine mashuhuri aliyehudhuria ukiondoa mabilionea na wamiliki wa makampuni makubwa duniani ikiwemo watangazaji wa CNN, CBS nk alikuwa ni Gayle King mtangazaji mashuhuri wa vipindi vya CBC Mornings na “King in the House”
Gayle kwa hapa Marekani ni mtu mashuhuri akijulikana pia kwa urafiki wake wa karibu na wa miaka mingi na nguli mwingine Oprah ambako pia yeye Gayle ni Mhariri wa jarida la Oprah la O Magazine!
Ends

Post a Comment