Serikali kupitia Wizara ya Elimu , Sayansi na Teknolojia imeahidi kuendeleza kazi nzuri ambayo Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza ya kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalum wanapewa fursa sawa kwa kuwapatia mahitaji wezeshi ikiwemo vitabu na vifaa maalum na saidizi vitakavyowawezesha kujifunza sawasawa na wanafunzi wengine kwa lengo la kuboresha ujifunzaji wao.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu , Sayani na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda wakati wa Uzinduzi wa kazi ya ugawaji wa vifaa na vitabu kwa kidato cha kwanza mpaka cha sita vya Breli na maandishi yaliyokuzwa pamoja na ugawaji wa vifaa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum wa vyuo vikuu .
Akizungumza katika Uzinduzi huo Profesa Mkenda amesema vitabu hivyo vinakusudiwa kusambazwa kwa wanafunzi 3,677 katika shule 764 za wanafunzi wasioona na wenye uwoni hafifu Tanzania Bara na Zanzibar.
Aidha Profesa Mkenda amesema mbali na vitabu hivyo serikali kupitia mpango huo wa maendeleo wa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya uviko – 19 imefanikisha kutoa kiasi cha shilingi milioni 770 kwa ajili ya kununua vifaa maalum na saidizi 413 kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum waliopo kwenye vyuo vikuu kumi na moja nchini
Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET ) Anneth Komba amesema vitabu vya Braili vimechapishwa nchini kupitia kiwanda pekee kilichopo hapa nchini chenye uwezo wa kuchapa vitabu vyenye maandishi ya Braili na mpaka sasa kupitia kiwanda hicho TET imesha chapa vitabu vyote vya Kiada vya elimu ya msingi pamoja na nyaraka za mitaala, huku mkurugenzi wa Elimu Maalum kutoka wizara ya elimu Sayansi na Teknolojia Dkt .Magreth Mathonya akiwataka wazazi wenye watoto wenye uhitaji maalum kuwapeleka shuleni badala ya kuwaacha nyumbani
Sanjari na hayo Serikali kupitia wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imeshauriwa kufanya sensa ya vijana na watoto wenye mahitaji maalum pamoja na kukagua miundombinu yao ili kufanikisha upatikanaji wa elimu sawa na sahihi kwa kila mtoto wa Kitanzania .

Post a Comment