Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt. Amos Nungu akizindua programu ya PesaTech Accelerator.
Baadhi ya washiriki katika uzinduzi wa programu ya PesaTech Accelerator.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na
Teknolojia (COSTECH) Dkt. Amos Nungu akiwa katika picha ya pamoja na wadau
mbalimbali wa sayansi na Tenknolojia.
................................
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na
Teknolojia (COSTECH) Dkt. Amos Nungu amezindua programu ya PesaTech Accelerator
inayolenga kukuza mawazo ya kibunifu kwa ajili ya mifumo ya Sekta ya Fedha
nchini.
Halfa ya uzinduzi huo imefanyika katika ukumbi wa ZO
Space (mkabala na Millenium Tower), jijini Dar es Salaam, ambapo Dkt. Nungu
amesema kuwa "Serikali kupitia COSTECH, tunajivunia kwa kuwa tumeendelea
kuweka mazingira wezeshi kwa wabunifu hapa nchini, program tuliyoizindua hii
leo itawasaidia wabunifu nchini kuongeza maarifa, kujenga mtandao, na kupata
fedha kwa ajili ya kuendeleza bunifu zao"
"Tarehe 4 Mei 2022, Mh. Rais katika
mahojiano na ndg. Mhando wa Azam TV, alisema jinsi ubunifu unavyowezesha vijana
kujiajili na kutoa ajira kwa wenzao ambapo aliitaja Magilla na Maxcom wakiwa ni
mfano wa wanufaika wa kumbi za bunifu kupitia COSTECH" amesema Dkt. Nungu.
Dkt. Nungu amewataka wabunifu wa mifumo ya kifedha
nchini kujitokeza kwa wingi katika kushiriki katika hiyo program ya PesaTech
Accelerator ili wapate fursa ya kujengwa na kuunganishwa na wafadhili
mbalimbali – kujenga kampuni changa nyingine mfano wa Nala inayoongozwa na
Benjamini Fernandes ambaye amepata uwekezaji wa Fedha za kimarekani milioni
kumi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Sahara Ventures,
Jumanne Mtambalike alieleza kuwa “Tutafanya kazi hii kwa karibu kabisa na
COSTECH, tuko hapa na Mkurugenzi Mkuu Dkt. Nungu vileivile tunashirikiana na
wadau muhimu kama UNCDF lengo likiwa ni kutambua vijana wenye mawazo
ya kibunifu kwa kuwapatia msaada wa kifedha, kiufundi, nyenzo pamoja
na msaada wa kibiashara ikiwemo kupatiwa mitaji ili mawazo yao yaingie sokoni
na kuleta tija katika jamii” alisema
Bi. Anneth Kasebele amesema kuwa Shirika la
Kimataifa la Mitaji - UNCDF kwa kushirikiana na Serikali na
makampuni binafsi wataendelea kusaidia miradi ambayo imejikita kwenye
mifumo ya kifedha na bunifu za mageuzi ya kidigitali kupitia sekta
za kifedha. Aliongeza kuwa dira yao ni kusaidia kuchochea jitihada zilizopo na
kupanua wigo wa huduma ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi wa Uendelezaji Masoko na Utafiti toka
Mamlaka ya Masoko, Mitaji na Dhamana (CMSA), Bw. Alfred Mkombo amesema kupitia
uzinduzi huo wabunifu katika sekta ya fedha nchini wataweza kusaidiwa kwa
kuendeleza mawazo yao eneo la fedha, masoko na mitaji na kwa kuendelea kutoa
miongozo itakayosaidia kutoa mawazo mapya yatakayoleta maendeleo
hapa nchini.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wadau wa ubunifu nchini wawezeshaji kwa maana ya UNCDF na Ubalozi wa Swedish; washirika wa mradi: Sahara Ventures, Enea Advisors, Hindsight Ventures ; pamoja na wadau wa Sekta za Kifedha zikiwemo Taasisi ya Flutterwave, CRDB, Mwalimu bank na Wabunifu wa Tunzaa, Tausi, na Bizzyn.



Post a Comment