Serikali kupitia Wizara ya Afya imewekeza fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya, ikiwemo hospitali za rufaa za mikoa ambapo, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawezi (Kilimanjaro) imeweza kutekeleza mradi wa ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Afya Catherine Sungura, wakati alipotembela miradi inayotekelezwa na Serikali kwenye hospitali hiyo.
“Kukamilika kwa ujenzi wa jengo hili litasaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto vitokanavyo na uzazi, jengo hili litakua na huduma zote zinazohitajika katika kila wodi, na pia kwa upande wa wagonjwa wa nje mama na mtoto ataweza kupata huduma zote hapa hapa” amefafanua Sungura.
Ametaja mradi mwingine katika hospitali hiyo ni ule wa ujenzi wa jengo la huduma za dharura ambapo, jengo hilo limekamilika kwa asilimia 95 huku tayari huduma za afya zikianza kutolewa katika jengo hilo lililogharimu zaidi ya shilingi milioni 764 ambalo pia litawekewa vifaa vya kisasa.
Kwa upande wa Jengo la wagonjwa mahututi Sungura amesema, Serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 149 kwa ajili ya ukarabati wa jengo hilo na hadi sasa utekelezaji huo umefikia asilimia 80.



Post a Comment