********************************
Na. WAF - Kigoma
Wananchi wametakiwa kuchukua hatua ili kuondokana na baadhi ya changamoto za hedhi na pia kuweza kusaidia kuondoa unyanyapaa au kutengwa kwa wasichana na wanawake kutokana na hali ambayo Mwenyezi Mungu amewaumba nayo ili kuendeleza kizazi kwa ajili ya maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Hayo ameyasema mke wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Mbonimpaye Mpango kwenye maadhimisho ya Hedhi salama Duniani ambapo kitaifa yamefanyika Mkoani Kigoma.
Mama Mpango amesema Kupitia utekelezaji wa Kampeni ya Taifa ya Usafi wa Mazingira mwaka 2020/21 Serikali imefanikiwa kujenga na kukarabati jumla ya vituo 878 kwa kuviwekea miundombinu ya maji na usafi wa mazingira katika Halmashauri 86 katika mikoa 17 nchini.
"mwaka 2020 imeonesha kuwa asilimia 66.8 ya shule ndizo zina huduma ya hedhi salama ambapo kati ya hizo zilizobainika kuwa na viteketezi ni asilimia 24, asilimia 22.8 zinatupa kwenye mashimo na asilimia19.5 zinachoma taka kwenye vichomea taka visivyokidhi vigezo." Amesema Mama Mpango
Hadi kufikia Machi 2022 ni asilimia 72.1 ya kaya zina vyoo bora na 52.8 zina vifaa vya kunawia mikono kwa maji tiririka; hii ni kwa mujibu wa taarifa za robo kutoka katika mfumo wa uingizaji na utoaji taarifa wa NSMIS.
Aidha amebainisha miongoni mwa changamoto zinatokana na Ongezeko la idadi ya wanafunzi haiendani na miundombinu iliyopo shuleni. Mfano matundu ya vyoo na sehemu za kunawia mikono hazitoshelezi mahitaji ya wanafunzi.
Pia, Ni asilimia 27.8 tu ya shule zina matundu ya choo yanayofikia kiwango cha ubora kulingana na mwongozo wa Wizara ya Elimu kwa uwianon wa 1:20 kwa wasichana na 1:25 kwa wavulana.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amesema Bila hedhi kwa mwanamke hakuna uzao hivyo ni wajibu wetu sote kuhakikisha upatikanaji wa taarifa, vifaa na mazingira wezeshi wakati wa hedhi.
Prof. Makubi amesema Ifikapo mwaka 2030 tunatarajia kuwe na ulimwengu ambao hakuna mwanamke au msichana atakayeachwa nyuma katika sekta yeyote kisa tu anapata changamoto ya kumudu gharama za taulo za kike, kupata maji salama na pamoja na vyoo bora.
"Katika kufanikisha hilo na kuhakikisha kunakuwa na ulimwengu ambao hakuna unyanyapaa wala ufukara katika suala zima la hedhi, kila mwanamke na msichana anahitaji kuwezeshwa kusimamia hedhi salama kwa ujasiri na bila aibu." Amesema Prof. Makubi
Hivyo, bado kuna umuhimu wa kuendelea kutoa elimu shuleni, katika jamii ikiwemo kwa kuwashirikisha wanaume ili waweze kufahamu kuhusu hedhi salama kwa ujumla wake.
Katika kufanikisha maadhimisho haya, shughuli mbalimbali zimefanyika ikiwa ni pamoja na kuendesha mdahalo Kisera wa Hedhi Salama, kufanya maonesho ya shughuli mbalimbali za masuala ya hedhi salama, na Mbio za kuchangia masuala ya hedhi salama.
Lengo la jitihada kwa serikali ni kuihamasisha jamii ili kuweza kuleta mabadiliko kwenye suala zima la Hedhi salama.


Post a Comment