Na Mwandishi Wetu
Wadau wa elimu ya juu wamepongeza mpango mpya wa serikali kuhamasisha vyuo vikuu kuanzisha kampasi za elimu ya ufundi.
Wamesema mpango huu utawezesha upatikanaji wa wahitimu wenye ujuzi na wanaohimili ushindani wa soko la ajira unaokuwa kwa kasi.
“Tunaipongeza serikali kwa kuwa na mpango wa kupanua wigo wa elimu ya ufundi kwa kuvitaka vyuo vikuu na taasisi zingine za elimu ya juu kufundisha kozi zinazotoa ujuzi kwa wahitimu ili waweze kustahimili ushindani wa soko la ajira,” alisema Bi Angela Mungai, mmoja wa wadau wa elimu ya juu katika mahojiano na mwandishi wetu.
Maoni ya wadau yanakuja baada ya taarifa ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda aliyoitoa bungeni hivi karibuni, akivita vyuo vikuu na taasisi zingine za elimu ya juu kuanzisha kampasi za elimu ya ufundi kama sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuboresha utoaji wa elimu inayowapa wahitimu uwezo wa ushindani watakao utumia katika soko la ajira nchini.
Akihitimisha hotuba ya makadirio ya wizara yake bungeni, Profesa Mkenda alisema serikali itahamasisha vyuo vikuu(vya Serikali na binafsi) kujenga kampasi za elimu ya ufundi katika mikoa mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa Waziri Mkenda mpango huu unakusudia kukuza utoaji wa elimu ya ufundi katika vyuo vikuu na taasisi zingine za elimu ya juu kwa kuwajengea wahitimu uwezo kwa kuwapa ujuzi unaotakiwa kwenye soko la ajira la dunia ya leo.
Kimsingi, Waziri alikuwa akijibu maoni ya muda mrefu ya wabunge na wadau wa elimu ya juu, ambao kwa nyakati mbalimbali wamekuwa wakionyesha haja ya kuwepo kwa vyuo vikuu na taasisi zingine za elimu ya juu kutoa wahitimu wenye ujuzi unaotakiwa kwenye soko la ajira lenye ushindani mkubwa.
“Tuna wahitimu wengi wenye matokeo mazuri sana, lakini baadhi yao hawawezi hata kuwasha mashine. Wawekezaji, makampuni makubwa na wanafanyabiashara hawawezi kujiweka kwenye hatari kuajiri waombaji wa kazi wasio na ujuzi kwa sababu tu wana vyeti vinavyoonyesha wamefaulu vizuri sana. Wanahitaji wafanyakazi wenye ujuzi,” alismema Bw Eric Shigongo, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Buchosa, wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Elimu bungeni.
Mohamed Unju, mbobezi wa maswala ya elimu ya juu amesema "soko la ajira linahitaji wahitimu wenye ujuzi wa kazi na siyo tu kuwa na shahada zinazoonyesha ufaulu mzuri. Tunafurahi kuona kwamba serikali imedhamiria kupanua wigo wa elimu ya ufundi hadi vyuo vikuu na taasisi zingine za elimu ya juu."
Ameongeza kuwa ili Tanzania iweze kunufaika na uwekezaji unaonendelea nchini katika sekta mbalimbali za uchumi, elimu ya ufundi ni lazima ipanuliwe badala ya kutolewa tu kwenye vyuo vya ufundi peke yake.
Wadau wa elimu ya juu wanatoa changamoto kwa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kurekebisha mwongozo unaozuia vyuo vikuu kufundisha kozi zilizo chini ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) zinazotoa ufundi wenye ushindani kwenye soko la ajira. Vyuo vikuu vinazuiwa pia kutoa kozi za elimu ya ufundi kwa ngazi ya stashahada na cheti, ambazo hazikuwepo kwenye utaratibu wa awali, hata kama zinawapa wahitimu ushindani unaotakiwa kwenye soko la ajira.
Wadau wa elimu ya juu wametaja kifungu 1.5 cha Mwongozo wa Elimu ya Juu Tanzania (Toleo la 3) la Mwaka 2019 uliotolewa na TCU mwezi Desemba mwaka 2020, kama moja ya vikwanzo vinavyozuia
vyuo vikuu na taasisi zingine za elimu ya juu kutoa kozi zinazowapa wahitimu ujuzi unaoendana na soko shindani la ajira, na kuomba TCU kurekebisha miongozo yake ili iendane na mpango mpya wa serikali.
Alipotafutwa, Msemaji wa TCU, Bi, Jorlin Kagaruki, alisema “Sisi TCU kama wasimamizi wa Vyuo Vikuuu hatuna tatizo lolote na mpango mpya wa Serikali unaolenga kuhamasisha Vyuo Vikuu (vya Serikali na Binafsi) kujenga au kuanzisha matawi/campus yatakayotoa Elimu ya Ufundi (Technical Education Campuses)…wala miongozo yetu (TCU haitazuia vyuo vikuu vinavyojenga au vinavyotaka kujenga matawi ya Elimu ya Ufundi, kama sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Serikali iliyotangazwa na Waziri Adolf Mkenda Bungeni.”
“TCU hatutakuwa kikwazo katika utekelezaji wa Mpango wa Serikali uliotangazwa n a Waziri,” amesema.
mwisho...

Post a Comment