*******************************************
Jumuiya ya Kujihami NATO imezialika Sweden na Finland kujiunga hii leo na muungano huo wa kijeshi, baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine kuzisukuma nchi hizo mbili kuachana na utamaduni wao wa kutoegemea upande.
Mataifa 30 washirika wa NATO wamechukua uamuzi huo katika mkutano wao wa kilele mjini Madrid, na pia wamekubaliana kuizingatia Urusi kama kitisho kikubwa zaidi na cha moja kwa moja kwa usalama wa washirika wake.
Baada ya mazungumzo ya masaa manne mjini Madrid jana Jumanne, rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alikubaliana na wenzake wa Finland na Sweden kuhusu hatua kadhaa za kiusalama kuyaruhusu mataifa hayo mawili ya Nordic kuepuka kura ya turufu ya Uturuki, ambayo Ankara iliiweka mwezi Mei kutokana na wasiwasi wake kuhusu ugaidi.
Waraka wa NATO pia umeitaja China kuwa mpinzani kwa mara ya kwanza, na kuweka mazingira kwa mataifa washirika kupanga kushughulikia mabadiliko ya China kutoka mshirika wa kibiashara hadi mshindani anaekuwa kwa kasi kubwa.
#Dwkiswahili

Post a Comment