Mratibu Kitaifa wa Mtandao Wa Watetezi Wa Haki Za Binadamu -THRDC Onesmo Ole Ngurumwa wakati wakizungumza na waandishi wa habari akitoa taarifa kuhusu kikao cha wadau wa haki za binadamu ambacho kimefanyika Juni 22 mwaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la kutetea na kuinua maisha ya Wafugaji
Tanzania Kamakia Robert akizungumza na waandishi wa habari akitoa
taarifa kuhusu kikao cha wadau wa haki za binadamu ambacho kimefanyika Juni 22 mwaka
huu.
..............................
NA MUSSA KHALID
Mtandao wa Watetezi wa
Haki za Binadamu nchini Tanzania –THRDC umeipongeza
serikali kwa kufungua mlango wa majadiliano kati ya asasi za kiraia na wizara
ya katiba na sheria kwa lengo la kutafuta ukweli juu ya mgogoro wa Loliondo na
Ngorongoro.
Hayo yameelezwa leo
jijini Dar es salaam na Mratibu Kitaifa wa Mtandao Wa Watetezi Wa Haki Za
Binadamu -THRDC Onesmo Ole Ngurumwa wakati wakizungumza na waandishi wa habari akitoa
taarifa kuhusu kikao cha wadau wa haki za binadamu ambacho kimefanyika Juni 22 mwaka
huu kwa lengo la kujadili haki za binadamu na zoezi la uwekaji mipaka Loliondo sambamba
na uhamaji wa hiari wakazi wa ngorongoro.
Mratibu huyo ameipongeza
serikali kwa jitihada za kuwaandalia mazingira rafiki wakazi wanaohama
kutoka eneo la hifadhi ya Ngorongoro kwa hiari huku wakiiomba kuendelea kuzingatia
usalama pamoja na kutumia njia sahihi za ushawishi kwa wakazi hao.
‘THRDC inaamini
kuwa njia bora ya utatuzi wa mgogoro wa Loliondo ni kuwa na majadiliano.
Tunaishukuru Wizara ya Katiba na Sheria na Idara zote za Serikali zilizoshiriki
katika kikao hicho muhimu kama mwanzo wa majadiliano ya kutafuta suluhu ya kudumu
katika eneno la Loliondo na Ngorongoro bila ukiukwaji wa haki za binadamu.’amesema Olengurumwa
Mtandao huo pia
umeishauri serikali kufanya tathmini na kupata idadi kamili ya wananchi waliokimbilia
nchi Jirani kwa ajili ya matibabu ili angalau waweze kurudi nchini na wahakikishiwe
kupatiwa matibabu hapa nchini.
Mtandao huo umewashauri
viongozi na wananchi waliokamatwa na kushtakiwa waachiwe huru na washiriki
katika mazungumzo ya maridhiano. Uchunguzi unaofanywa kuhusu kesi ya mauaji ya
Askari wa Jeshi la Polisi ufanyike bila kuathiri watu wasiokua na hatia.
Kwa upande wao Mkurugenzi Mtendaji
Shirika la kutetea na kuinua maisha ya Wafugaji Tanzania Kamakia Robert pamoja
na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo Jumuishi Ngorongoro Loselia Maoi
wameiomba serikali kuwachukulia hatua za wale wote waliohusika na mauaji
ya askari wa jeshi la polisi aliyeuawa kwa mshale Juni 11 mwaka huu huku
wakiishauri serikali kulipitia upya shauri la mauaji hayo linalowakabili viongozi
kumi wa kijamii wanaodaiwa kuhusika mauaji hayo.
Wamependekeza viongozi
na wananchi waepuke kuendelea kutoa kauli za kibaguzi na badala yake waendelee
kujenga umoja na kuaminiana katika kutafuta suluhu ya migogoro ya ardhi katika
Wilaya ya Ngorongoro.
Hata hivyo Watetezi hao wameishauri serikali kuweka mazingira rafiki ya utendaji kazi kwa vyombo vya habari nchini katika mgogoro wa eneo la hifadhi ya taifa ya Ngorongoro ili kuepusha kuchafua taswira ya nchi kwa mataifa mengine kutokana na vyombo vya nje kuripoti taarifa ya mgogoro huo kinyume na uhalisia hali wake



Post a Comment