**********************************************
Timu ya kina dada wa Ujerumani imefaulu kuingia kwenye robo fainali katika mashindano ya kandanda ya kugombea ubingwa wa mataifa ya Ulaya kwa wanawake baada ya kuilaza Uhispania mabao 2-0.
Kilele cha uhondo wa soka hapo jana usiku lilikuwa pambano kati ya Uhispania na Ujerumani. Hapakuwa na haja ya kupiga ramli ili kujua matokeo.Licha ya kuingia na matuamaini ya juu kwenye uwanja wa mji wa Brentford, wahispania hawakufua dafu mbele ya Ujerumani.
Akina dada wa Uhispania walijiuma vidole katika dakika ya tatu baada ya mlinda lango wao kufanya kosa ambalo hatalisahau maisha yake yote. Alitoa zawadi kwa Ujerumani. Golikipa huyo alitaka kutoa pasi kwa beki wake lakini boli lilienda moja kwa moja kwenye miguu ya fowadi wa Ujerumani karibu na lango la Uhispania na akaujaza mpira wavuni. Maafa kwa wahispania yaliendelea katika dakika ya 36 ambapo wajerumani walijipatia goli la pili la kichwa.
Ushindi huo maana yake Ujerumani itaingia mapema katika robo fainali ambapo itakutana na Finland hapo jumamosi. Leo jioni Uswisi itakumbana na Sweden na waholanzi watakuwa na miadi na timu ya akina dada wa Ureno.
Katika mechi ya ufunguzi kina dada wa Denmark waliangukia patuputu pale walipoumbuliwa na Ujerumani kwa kipigo cha mabao manne kwa bila, lakini hapo jana walipania katika mchezo wao dhidi ya timu ya Finland ambao pia waliadhibiwa na Uhispania kwa kubandikwa mabao manne kwa moja, katika mchezo wao wa kufungua dimba.
Dwkiswahili

Post a Comment