CHAMA cha mapinduzi (CCM) wilayani Kakonko mkoani Kigoma,kinatarajia kutoa tuzo ya heshima kwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo baada ya kushika nafasi ya kwanza kwa ukusanyaji mapato.
Akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani Mwenyekiti wa CCM wilayani humo,Saamoja Sadock,amesema ofisi ya mkurugenzi mtendaji pamoja na watendaji wengine idara za halmashauri hiyo wamefanya kazi kubwa sana kuhakikisha ukusanyaji mapato ya serikali unafanikiwa.
"Kazi iliyofanywa na Mkurugenzi wetu Stephano Ndaki, inahitaji kupongezwa sana...hii inatia moyo kuwa wilaya yetu ya kokonko inasonga mbele kimaendeleo...sisi kama chama cha mapinduzi tutamuandalia tuzo ya heshima kwa kazi hii kubwa aliyofanya ikiwa ni ishara ya hamasa ya kuendelea zaidi ya hapo"amesema Sadock.
Kauli hiyo imekuja baada ya Kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo,Christopher Bukombe, kusoma taarifa ya ukusanyaji mapato ya ndani kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2021/22 ambapo halmashauri hiyo imeshika nafasi ya kwanza kati ya halmashauri nane za mkoa wa Kigoma.
Pia imefanikiwa kushika nafasi ya 15 kitaifa kati ya halmashauri 184 zilizopo nchini kutokana na kuvuka lengo la makusanyo baada ya kukusanya aslimia 102.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Fidelis Ndelego,akasema mafanikio ya ukusanyaji huo yametokana na mshikamano mzuri kati ya madiwani na watumishi wa halmashauri ambao wanasukumwa na ufanyaji kazi kwa uzalendo wa hali ya juu.
"Mafanikio tuliyoyapata hatuna budi kujivunia haikuwa kazi rahisi kufikia malengo na kuvuka... siri kubwa ya mafanikio haya ni mshikamano mzuri kati yetu madiwani pamoja na watumishi wa halmashauri...tunaahidi kufanya vizuri zaidi kuliko tulivyofanya awamu hii"amesema Ndelego.
Rehema Deus,mkazi wa Kakonko amesema ukusanyaji mzuri wa mapato ya ndani kwa halmashauri hiyo itaongeza chachu ya maendeleo kwa wananchi, kutokana na halmashauri kutumia fedha zake kwa miradi ya jamii badala ya kungoja fedha toka serikali kuu.
Mwisho.


Post a Comment