****************************
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imeipongeza TMDA kwa kazi kubwa ya udhibiti inayofanyika katika kulinda Afya ya Jamii na kuzitaka taasisi zingine chini ya Wizara ya Afya kuiga mifumo ya utendaji iliyopo katika mamlaka hii.
Hayo yamebainishwa na wajumbe wa kamati hiyo kwa nyakati tofauti wakati wakichangia na kujadili taarifa ya Utendaji Kazi ya TMDA kwa mwaka 2021/22 iliyowasilishwa bungeni Dodoma tarehe 1 Septemba, 2022.
Hata hivyo Wito umetolewa kwa TMDA kuendelea kuimarisha udhibiti katika vituo vya forodha huku mjazo ukiwa ni kusimamia na kuwezesha viwanda vya ndani vya dawa kuzalisha dawa salama, bora na fanisi.
Aidha, TMDA imetakiwa kuweka mkakati na kuimarisha utoaji elimu kwa wananchi kuanzia ngazi ya kijiji ili wananchi wapate taarifa muhimu juu ya matumizi sahihi ya dawa na vifaa tiba.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Aloyce Kamambwa ameishauri TMDA kuungana na taasisi nyingine za Serikali katika kufanya tafiti mbalimbali za masuala ya Afya na kuwezesha upatikanaji wa suluhisho juu ya magonjwa mbalimbali ambayo si ya kuambukiza yanayoshamiri kwa sasa.
Na kwa upande wake Naibu waziri wa Afya Dkt, Godwin Mollel wakati akiishukuru Kamati ya Bunge amesema wizara inaendelea kutathmini huduma ya tiba mitandaoni kabla ya kuiruhusu kuanza kufanyika nchini kutokana na mazingira ya nchi yetu.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Bw, Adam Fimbo wakati akiwasilisha taarifa ya utendaji Kazi mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge amesema Mamlaka pamoja na kutekeleza majukumu yake ya msingi kwa mwaka 2019/20 hadi 2021/22 imeweza kutoa gawio la takriban TSH, Bilioni 14.4 katika mfuko mkuu wa Serikali, na kwamba hesabu za TMDA zimekuwa zikikaguliwa kila mwaka na kupata hati safi kwa miaka 18 mfululizo sasa.



Post a Comment