Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa akizungumza na waombolezaji alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Samia
Suluhu Hassan kuaga mwili wa marehemu Balozi Paul Rupia, katika viwanja vya
Karimjee, Jijini Dar es Salaam Septemba 23, 2022 (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
.................................
WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amesema Serikali inatambua mchango mkubwa uliotolewa na marehemu
Balozi Paul Rupia wakati wa utumishi wake na hata baada ya kustaafu.
“Moja ya jambo
ambalo halitasahaulika ni uthubitu wake wa kuanzisha Benki ya Watu wa Dar es
Salaam (DCB) ambayo alikuwa mwenyekiti wake na hadi anaondoka katika
uongozi aliicha benki hiyo ikiwa na matawi manane na moja kati ya hayo likiwa
jijini Dodoma.”
Mheshimiwa Majaliwa
amesema hayo leo Ijumaa (Septemba 23, 2022) alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais
Samia Suluhu Hassan katika kuuaga mwili wa marehemu Balozi Paul Rupia, katika
viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam.
“Mheshimiwa Rais
Samia amenituma kuja kumuwakilisha katika msiba huu, amesema amepokea kwa
masikitiko taarifa za kifo cha Balozi Rupia, hakuweza kuhudhuria kwa
sababu yupo nchini Msumbiji kwa ziara ya kikazi. Pia ametoa pole kwa
familia na waombolezaji wote.”
Mheshimiwa Majaliwa
amewasihi Watanzania kumuombea marehemu na familia yake kwa Mwenyezi
Mungu ili apate pumziko la milele na familia iwe na ustahimilivu katika
kipindi hiki kigumu cha majonzi.
Kwa upande wake, Waziri
Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba amesema marehemu Balozi Rupia alichangia kwa
kiasi kikubwa mageuzi ya uchumi nchini na kuanzisha mageuzi ya kisiasa ya mfumo
wa vyama vingi nchini.
Awali, Mwenyekiti wa Mabalozi Wastaafu wa Tanzania, Balozi James Msekela amesema marehemu Balozi Rupia atadumu katika historia ya Tanzania kama mwanasiasa mahiri na mwanadiplomasia nguli.



Post a Comment