............................
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema serikali imeridhia kutungwa kwa sheria ya kulinda taarifa binafsi ambayo kwa mara ya kwanza sheria hiyo itasomwa katika mkutano wa Bunge utakaoanza Septemba 13 mwaka huu.
Waziri Nape ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam katika mkutano wa wadau wa mawasiliano na TEHAMA Connect to Connect Afrika ambapo ametoa rai kwa wadau mbalimbali kushirki kutoa maoni juu ya sheria hiyo itakayolinda faragha za mtu katika mawasiliano.
Aidha washiriki katika mkutano huo akiwemo Mkurugenzi wa Masuala ya kisekta Mamlaka ya mawasiliano Tanzania TCRA Emmanuel Manase na Mkurugenzi Mawasiliano na Uhusiano Vodacom Ropheline Moria kwa pamoja wamesema uwepo wa sheria ya kulinda taarifa binafsi katika mawasiliano itaweka mazingira salama kati ya watoa huduma za mawasiliano pamoja na watumiaji wa huduma hizo.
Mkutano huo wa wadau wa mawasiliano Africa umewakutanisha watunga Sera, Wadhibiti, Watoa Huduma na wawekezaji huduma za mawasiliano kutatathmini ajenda za Kitaifa za Maendeleo na Miradi ya Kuunganisha mtandao wa intaneti kati ya nchi na nchi kote barani Afrika.

Post a Comment