TMA YAENDELEA KUWASISITIZA WAKULIMA KUTUMIA TEKNOLOJIA YA KISASA KATIKA KILIMO MSIMU WA MVUA ZA VULI 2022.



Mchambuzi wa Hali ya hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini –TMA Rose Senyagwa akizungumza kwenye kipindi cha Morning Kiss ya Kiss Fm jijini Dar es salaam katika mada isemayo kuelekea msimu wa mvua za Vuli mwaka 2022,athari zipi zinaweza kujitokeza.

................................

NA MUSSA KHALID –KISS FM

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania –TMA imeendelea kuwasisitiza wakulima kuhakikisha wanatumia njia za kitaalamu za teknolojia ya kisasa katika kilimo ili kuendana na mabadiliko ya mifumo ya hali ya hewa katika Msimu wa mvua za Vuli mwaka huu.

Hayo yameelezwa jijini Dar es salaam na Mtaalamu na Mchambuzi wa Hali ya hewa kutoka TMA Rose Senyagwa wakati akizungumza kwenye kipindi cha Morning Kiss ya Kiss Fm katika mada isemayo kuelekea msimu wa mvua za Vuli mwaka 2022,athari zipi zinaweza kujitokeza.

Senyagwa amesema kuwa kutokana na Mvua za Vuli mwaka 2022 kutarajiwa kuwa za Chini ya Wastani hadi Wastani katika maeneo mengi ni vyema Wakulima wakaendana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kuepuka kulima kwa mazoea.

‘Kwa mwaka huu baada ya utabiri kutoka kwamba mvua zitakuwa chache au chini ya wastani katika maeneo mbalimbali wataalamu wa kilimo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya hewa wametoa ushauri kwamba wakulima kwa kipindi hiki watumie  utaalamu na waendane na mabadiliko ya tabia nchi’amesema Senyagwa

Aidha ameishauri jamii kuwa na tabia ya kuhifadhi chakula na maji kwa uangalifu katika ngazi ya kaya na taifa ili kuweza kuepukana na changamoto katika msimu huo.

Aidha  akizungumzia sekta ya maji amesema Upungufu wa kina cha maji katika mito, mabwawa na hifadhi ya maji ardhini unatarajiwa hivyo mamlaka husika zimeshauriwa kuwa na mipango madhubuti ya uzalishaji nishati ya umeme kutoka vyanzo vingine tofauti na maji kama jua, upepo na gesi.

‘Vyanzo vingi vya maji hutegemea zaidi mvua kuwa inaponyeesha kile kina cha maji kinaongezeka na maji yanaongezeka ya na kunapokuwa hakuna mvua maji yanatumika hivyo levo ya maji inazidi kushuka’ameendelea kuelezea Senyagwa

Vilevile ameikumbusha jamii kuhifadhi maji ili hali inapokuwa mbaya zaidi wanapata msaada kupitia maji waliyoyahifadhi.

Hata hivyo amewashauri watumiaji wa taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na wakulima, wafugaji, Mamlaka za Wanyamapori, Mamlaka za Maji na Afya waendelee kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalamu katika sekta husika.

0/Post a Comment/Comments