UNYWAJI WA POMBE HATARI KWA AFYA YA MOYO

 




Na Daniel Limbe, Kibaha

WAKATI Tanzania ikiungana na nchi zingine kuadhimisha siku ya Moyo duniani, imeelezwa kuwa watumiaji wa pombe kupita kiasi wapo katika hatari kubwa ya kukumbwa na ugonjwa huo.

Mbali na pombe,matumizi ya dawa za kulevya,dawa za kusisimua misuli,ulaji holela pamoja magonjwa ya kisukari vinatajwa kuwa kichocheo cha jamii kukubwa na maradhi hayo.

Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo,kutoka hospital ya rufaa ya kanda Chato,Dk. Marygoretti Changalucha, amesema hayo kwa njia ya simu wakati akizungumza na mwandishi wetu aliyetaka kujua mpango mkakati wa kupambana na magonjwa wa moyo nchini.

Daktari huyo,amesema unywaji wa pombe kupita kiasi umekuwa kichocheo cha ongezeko la magonjwa ya moyo katika jamii huku baadhi ya familia maskini wakishindwa kufika kwenye huduma za afya mapema.


Hata hivyo amedai kuwa unywaji wa kawaida ni ule ambao mwanaume hutumia bia zisizozidi 21 kwa wiki huku mwanamke akipaswa kunywa chupa 14 kwa wiki na kwamba kuzidi kiwango hicho nikuanza kuhatarisha afya ya mtumiaji.

"Tunashauri kwa mwanaume asizidi chupa tatu kwa siku ambazo ni sawa na chupa 21 kwa wiki huku mwanamke akipaswa kutumia chupa mbili ambazo ni sawa na chupa 14 kwa wiki"amesema Dk Changalucha.

Sambamba na hilo,ameitaka jamii kuachana na matumizi ya dawa za kulevya kwa madai kuwa nyingi huwa na chembechembe za sumu ambazo ni hatari kwa afya ya moyo huku akidai kuwa wenye magonjwa ya kisukari nao wapo katika hatari ya kukumbwa na ugonjwa huo hatari.

Aidha ametumia fursa hiyo kuiasa jamii kujenga utamaduni wa kupima afya zao kabla ya kuugua na kwamba hatua hiyo inaweza kuwaondoa katika hatari ya kutumia gharama kubwa kwenye matibabu na hata kifo.


                       Mwisho.

0/Post a Comment/Comments