WAZIRI BASHUNGWA APIGA MARUFUKU WALIMU KUPITA KILA OFISI YA HALMASHAURI KUTAFUTA HUDUMA.

 





Xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa amepiga marufuku walimu  kupita kila Ofisi ya Halmashauri  kutafuta  huduma na ameagiza   wapelekewe huduma hizo shuleni badala ya watoa huduma kufatwa. Ofisini.

Ametoa agizo hilo leo tarehe 8 Septemba, 2022 Jijini Dodoma wakati akiongea  na waandishi wa habari kutoa taarifa kwa umma ya uboreshaji wa huduma  kwa walimu nchini.

“Ni marufuku  kuwaacha walimu kupita kila ofisi ya Halmashauri kutafuta huduma, narudia tena mwalimu apelekewe huduma shuleni badala ya watoa huduma kukaa ofisini” amesema Bashungwa

Amesisitiza kuwa Mwalimu akiandika barua kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhitaji huduma, anapaswa kujibiwa kwa maandishi ndani ya siku 7 baada ya kupokelewa.

Aidha, Bashungwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote nchini kuwasimamia  Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Maafisaelimu, Maafisa wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Wathibiti Ubora wa Shule kuhakikisha wanawafuata walimu mashuleni  na kutatua kero na malalamiko yao kwa wakati.

Amewataka viongozi hao kufuatilia na kuwasimamia viongozi wa elimu katika ngazi ya Mikoa, Halmashauri, Kata na shule kutekeleza mikakati ya uboreshaji na usimamizi wa elimu na kuhakikisha wanawasilisha  taarifa ya utekelezaji   Ofisi ya Rais – TAMISEMI kila robo mwaka.

Vile vile, amewataka kusimamia utekelezaji wa Mipango ya Mafunzo kazini kwa walimu, kwa mujibu wa Mwongozo uliotolewa na Katibu Mkuu Utumishi na ufanyike kwa uwazi na ushirishwaji wa kutosha, ili kuondoa dhana ya kuwa waajiri wanatoa nafasi za mafunzo kwa upendeleo.

Pia, Bashungwa amewaelekeza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwasimamia Maafisa wa Tume ya Utumishi wa Walimu kuzingatia miongozo ya upandishwaji vyeo walimu, ili kila anayestahili kupandishwa cheo, anapandishwa kwa mujibu Sheria, Kanuni na Miongozo.

0/Post a Comment/Comments