Xxx xxx xxxxxxxxxxxcxxxxxxx
Na Daniel Limbe,Kibaha
RAIS mstaafu wa Tanzania,Jakaya Kikwete, amedai pasipo kuwa na mazingira ya uwekezaji nchini ni ndoto kuufikia uchumi imara.
Mbali na hilo ameufagilia mkoa wa Pwani kuwa ndiyo sehemu sahihi ya kuwekeza viwanda kutokana na kuwa na maeneo mengi ya uwekezaji,ukilinganisha na mkoa wa Dar es salaam ambao umejaa.
Ameyasema hayo leo wakati akizindua wiki ya maonesho ya 3 ya uwekezaji na biashara kwenye mkoa huo,huku akiishauri serikali kutogawa ardhi yote kwa wawekezaji na kuwasahau wananchi wakiwemo maskini.
Amesema mbali na serikali kuwa na mpango mzuri wa kupima ardhi kwaajili ya kuwavutia wawekezaji,ipo haja kubwa ya kupima viwanja vya kuwauzia wananchi maskini badala ya kujikita kwa matajiri pekee.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa mkoa wa Pwani,Abubakari Kunenge, amedai kuwa mkoa wa Pwani unaongoza kwa wingi wa viwanda nchini ambapo una jumla ya viwanda 1,460 na kati yake 90 ni viwanda vikubwa.
Kadhalika mkoa huo unavivutio vya utalii zaidi ya 70 huku akiwataka wawekezaji kufika mkoa wa Pwani kuwekeza viwanda vyao eneo hilo badala ya kwenda maeneo mengine.
Na kwamba uwepo wa viwanda hivyo umepunguza tatizo la ajira kwa vijana waliokuwa wakitaabika mtaani huku akiwataka wamiliki wa viwanda hivyo kufanya malipo yao ndani ya mkoa huo ili kusaidia ongezeko la mapato yatakayosaidia kutekeleza miradi mingi ya maendeleo ya wananchi wa mkoa wa Pwani.
Aidha Kunenge amesema, Mkoa huo umejipanga vizuri kutekeleza sera ya serikali ya uwekezaji kwa lengo la kuwavutia wawekezaji wengine.
Kwa upande wake, Mkurugenzi mkuu shirika la maendeleo ya kuhudumia viwanda vidogo (Sido),Silvester Mpanduji, amesema shirika hilo limefanikiwa kuwakutanisha wajasiliamali wa ukanda wa Pwani,kubadilishana uzoefu na sekta mbalimbali,kwa lengo la kuwainua wananchi wa chini.
Hata hivyo Prof. Mpanduji amesema huduma za Sido zimeongeza ari ya wananchi kuanzisha viwanda kwenye maeneo yao,na kwamba zaidi ya viwanda vidogo 247 vimeanzishwa nchini.
Aidha shirika hilo limeomba kuendelea kuwezeshwa na serikali ili liweze kutimiza ndoto zake kwa lengo la kufikia azma ya serikali kuwa na nchi ya viwanda.
Maonyesho hayo yamefanyika leo yakiwa yametanguliwa na mengine ya mwaka 2018/19 pamoja na 2019/20.
Mwisho.




Post a Comment