MAGONJWA SUGU CHANZO CHA AFYA YA AKILI

 


Picha ya ugonjwa wa saratani...kwa hisani ya mtandao

Xxxxxxxxxxxxxx


Na Daniel Limbe, Dar es salaam

IMEELEZWA kuwa magonjwa sugu ya binadamu ni miongoni mwa sababu zinazochangia ongezeko la afya ya akili nchini.

Miongoni mwa magonjwa hayo ni pamoja na Ukimwi,Kisukari, shinikizo la damu na Kansa, huku mapenzi yasiyo salama nayo yakitajwa.

Hayo yamebainishwa na daktari Bingwa wa afya ya akili kutoka hospitali ya taifa ya Mhimbili,Dk. Said Kuganda,wakati akijibu maswali ya baadhi ya waandishi wa habari za afya ya akili kupitia kundi sogozi.

Amesema jamii inapaswa kutambua kuwa ugonjwa wa akili unatibika na kwamba kuna haja ya jamii kuwapeleka hospitali haraka watu wenye dalili za ugonjwa huo kwaajili ya uchunguzi na tiba.

"Nashauri watu wenye dalili za afya ya akili wapelekwe mapema kwenye vituo vya kutolea tiba kwaajili ya uchunguzi na tiba badala ya kuendekeza imani za kishirikina"amesema Kuganda.

Kwa upande wake,mtaalamu wa saikolojia, Saldin Kimangale, amesema aslimia 50 ya watu wenye ugonjwa wa akili huwakumba wakiwa chini ya miaka 14 na kwamba hutambulika baadaye kutokana na jamii kutokuwa na utamaduni wa kupima afya kabla ya kuugua.

Hata hivyo,amesema siyo kila anayezungumza peke yake ana ugonjwa wa akili,ispokuwa yaweza kuwa dalili za ugonjwa huo ambapo mtu husikia sauti ambazo wengine wasikii au anaona vitu ambavyo wengine hawaoni.

"Mtu akipata ugonjwa wa akili siyo rahisi yeye kujitambua kama ni mgonjwa ispokuwa wengine kwa sababu kiungo cha utambuzi ndicho kinachokuwa kimepata madhara"amesema Kimangale.

Kadhalika amesisitiza kuwa ugonjwa wa akili unatibika,na kwamba hatua hiyo itasaidia kupunguza ongezeko la watu kufanya uamuzi usiotarajiwa ikiwemo kujeruhi, kuua na hata kujinyonga.

Kwa mujibu wa takwimu za shirika la Afya duniani (WHO) zilionyesha kuwa kufikia mwaka 2020 zaidi ya watu bilioni moja walikuwa wakiishi na magonjwa ya akili wakiwemo vijana wa kati ya miaka 15 hadi 39.


                         Mwisho.

0/Post a Comment/Comments