RAIS SAMIA AAHIDI KUISHI GEITA




 Na Daniel Limbe,Chato

KATIKA Kile kinachoonekana rais Samia Suluhu kuvutiwa na amani, utulivu na mazingira mazuri ya mkoa wa Geita,ameahidi kuwa mkazi wa mkoa huo kwa muda usiojulikana.

Kauli hiyo ameitoa kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na baadhi ya wananchi wa wilaya ya Chato muda mfupi baada ya kutembelea hospitali ya rufaa ya kanda Chato na baadaye katoro wilayani Geita.

"Naomba nirudie kauli yangu niliyoitoa kule chato baada ya kutembelea hospitali kubwa ya rufaa ya kanda...mimi ni mwana geita na ninawaahidi nitakuja kuishi mkoani geita muda frani" amesema na kushangiliwa na umati wa wananchi.

Aidha rais Samia amewapongeza wananchi wa wilaya ya Chato na mkoa wa geita kwa kuendelea kuchapa kazi huku akiwasisitiza kuongeza kilimo cha mpunga na mazao mengine ili kujikwamua kiuchumi.

Mbali na wananchi akatumia fursa hiyo kuwapongeza wabunge wa mkoa wa geita kwa kuwasilisha kwake mahitaji ya wananchi na kwamba serikali inaendelea kuchukua hatua kutatua changamoto mbalimbali za wananchi ikiwemo uwekaji wa taa za barabarani,barabara za lami na zile za mitaa.

Rais Samia amewasili leo (jana) wilayani Chato kwa ziara ya kikazi baada ya kutoka mkoani Kagera kwenye sherehe za kilele cha mbio za mwenge na wa uhuru kitaifa zilizoambatana na kumbukizi ya miaka 23 ya kifo cha muasisi wa taifa Hayati mwl. Julius Kambarage Nyerere.

Pia akiwa wilayani Chato,ametembelea kaburi la Hayati rais Dk. John Magufuli nyumbani kwake Rubambangwe Mlimani kisha kumsalimia mama mzazi ya hayati Magufuli,mama Suzan Joseph kabla ya kuelekea hospitali ya rufaa ya kanda Chato.

Akizungumza na mwandishi wetu,Hamis Mwitazi(mkazi wa chato kati) mbali na kumpongeza rais Samia kwa uamuzi wake wa kufanya ziara ya kikazi wilayani humo,amesema hatua hiyo inafufua matumaini ya kutekeleza miradi ya maendeleo iliyoanzishwa na Hayati rais Dk.Magufuli.

"Ukweli ni kwamba ujio wa rais Samia hapa wilayani kwetu unaendelea kutupa matumaini makubwa ya kwamba atatekeleza miradi yote iliyokuwa imeanzishwa na mtangulizi wake Dk. Magufuli" amesema Mwitazi.

Naye Mbunge wa Jimbo la Chato,Dk. Medard Kalemani, ametumia fursa hiyo kumpongeza rais Samia kwa jitihada kubwa za kuiongoza nchi na kudumisha amani na mshikamano huku akimuahidi kutembea kifua mbele kutokana na wananchi wa jimbo hilo kumuunga mkono.

                        Mwisho.

0/Post a Comment/Comments