Na: Issa Mohamed.
Mganga mkuu wa serikali Dkt Aifello Sichalwe amewataka watafiti wa Afya nchini kuzingatia kanuni na maadili ya utafiti ili kuleta matokeo chanya kwa maslahi mapana ya ulinzi na ustawi wa jamii kwa maendeleo ya Taifa.
Dkt Sichalwe ametoa agizo hilo Jijini Dar es salaam wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku nne yenye lengo la kuboresha kanuni na maadili ya tafiti za kitabibu pamoja na uwezo wa kudhibiti tafiti katika nchi takribani tano ikiwemo Rwanda, Kenya, Uganda, Malawi na Tanzania.
Amesema kufanya tafiti kwa kuzingatia miiko ya utumishi umma itasaidia kuzalisha matokeo yenye tija ikiwemo kuandaa miongozo hivyo taasisi za kitaaluma zinapaswa kuendelea kutoa mafunzo ili kupambana na magonjwa mbalimbali.
‘’Kama hakutokua na maadili hata yale matokeo tutakayoyapa yatakua yauongo, watafiti mnapawa kuzingatia kanuni na maadili ili kuleta matokeo yenye ushahidi’’ Amesema Dkt Sichalwe
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Taifa ya utafiti magonjwa ya Binadam nchini –NIMR, Dkt William Kisinza amesema mafunzo hayo yatasadia kujenga uwezo katika tafiti nchini.
‘’Mafunzo ya leo yamekutanisha nchi tano zinazotoa uwezeshaji wa hawa wanaosimamia maadili ya utafiti, kwahiyo mimi kama msimamizi mkuu wa utafiti haya mafunzo ni muhimu sana’’ Amebainisha Dkt William Kisinza
Nao baadhi ya wadau waliohudhuria mkutano huo wamesema kuwa matatizo ya Afya yanazidi kuongezeka hivyo mkutano huo utaleta ujumuishi katika maswala ya tafiti.
Taasisi ya taifa ya utafiti magonjwa ya Binadam –NIMR imepewa majukumu mbalimbali ikiwemo kufanya utafiti pamoja na kuratibu tafiti nchi nzima pia kusimamia maadili ya utafiti za afya nchini.




Post a Comment