Mita ya Dawasco iliyokaguliwa na WMA na kuwekwa siri (yenye rangi ya karoti) ili kuthibitisha ubora wa huduma kwa watumiaji maji.
Mwandishi wetu,Daniel Limbe,akipata maelezo ya namna WMA inavyotekeleza majukumu yake
Xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na Daniel Limbe,Kibaha
WAKALA wa vipimo nchini (WMA) imewataka wananchi wenye malalamiko ya kutozwa kiasi kikubwa cha fedha za utumiaji maji majumbani kinyume na matumizi halisi, kupeleka changamoto hiyo kwao ili kuhakiki iwapo mita za maji wanazotumia zimehakikiwa na mamlaka hiyo.
Aidha Mamlaka hiyo imesema inalojukumu la kukagua mita za maji, umeme,mizani ya kununulia madini,pamba,kahawa,korosho pamoja na ile inayotumika kupima bidhaa mbalimbali kwenye maduka ya jumla na lejaleja kisha kuweka alama ya siri kuthibitisha kuwa kipimo hicho ni sahihi kwa matumizi.
Akizungumza na mwandishi wetu kwenye maadhimisho ya 3 ya wiki ya uwekezaji na Biashara mkoani Pwani, Ofisa mwandamizi wa wakala wa vipimo mkoa huo,Gaudence Gaspar, mesema lengo la wakala hiyo ni kuhakikisha wanamlinda mlaji kwa kudhibiti bidhaa zilizofungashwa chini ya kiwango au juu ya kiwango.
"Tunalazimika kuhakikisha mlaji anapata kile kinachotakiwa kulingana na thamani ya pesa yake yake...pia mtoa huduma afaidike kwa haki ya kiwango anachotakiwa kukitoa kwa mlaji" amesema Gaspar
Aidha amedai kutumia huduma za Mzani pasipo kukaguliwa ni kinyume na sheria ya vipimo sura namba 340 iliyofanyika mapitio mwaka 2002 ambayo inamtaka kila mtoa huduma kuhakikisha vipimo anavyotumia lazima viwe vimehakikiwa na mamlaka hiyo.
Na kwamba iwapo mtoa huduma akithibitika kukiuka sheria hiyo anaweza kupata adhabu inayoanzia shilingi laki 1 na isiyozidi 20 milioni.
Gaspar amedai kuwa iwapo mtumiaji huduma ya maji akibaini mita yake imefungwa kuanzia mwaka 2020 na haina siri ya uhakiki uliothibitishwa na WMA, anapaswa kutoa malalamiko yake kwa wakala hiyo ambayo itamtaka mtoa huduma kuwajibika na vipimo vyake.
Kwa upande wake, Loyce Katemba,mkazi wa kata ya sofu Kibaha,amesema awali hakuwa na ufahamu iwapo mita za maji hutakiwa kuhakikiwa na wakala wa vipimo nchini,na kwamba hali hiyo itasaidia kuondoa kero kwa jamii iwapo wananchi wataelimishwa na kuelewa umuhimu wa WMA.
Mwisho.


Post a Comment