DCEA YAMKAMATA MTUHUMIA AKIWA NA BISKUTI 50 ZILIZOTENGENEZWA KWA DAWA ZA KULEVYA AINA YA BANGI

Kamishna Jenerali wa DCEA, Gerald Kusaya

.......................

NA MUSSA KHALID

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa Za kulevya - DCEA imemkamata Mtuhumiwa Abdulnasir Kombo (30) mfanyabiashara mkazi wa Kaloleni jijini Arusha akiwa na Biskuti 50 zilizotengenezwa kwa kutumia dawa za kulevya aina ya Bangi kama malighafi akiwa anaziuza kwenye eneo hilo.

Pia Mamlaka hiyo imesema katika tukio hilo imefanikiwa kumkamata mtuhumiwa mwingine Hassan Ismail Mkazi wa Olasiti jijini Humo anayesadikiwa kuwa ndiye mtengenezaji wa biskuti hizio zenye dawa za kulevya.

Hayo yameelezwa jijini Dar es salaam na  Kamishna Jenerali wa DCEA, Gerald Kusaya ambapo amesema hayo yamejiri kufuatia operesheni endelevu wanazozifanya katika maeneo mbalimbali nchini na hivyo watuhumiwa wote wamefikishwa mahakamani jijini Arusha.

“Uwepo wa bidhaa za vyakula vinavyotengenezwa kwa kutumia bangi vimeanza kushamiri hapa nchini, itakumbukwa mwaka 2020-2021 mamlaka ilikamata bangi iliyosindikwa mfano wa jam, Keki na Asali katika matukio tofauti,” amesema Kamishna Kusaya

Aidha Kamishna Jenerali Kusaya amesema katika kipindi cha mwezi Oktoba na mwanzoni mwa mwezi Novemba Mamlaka hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama wamefanya operesheni maeneo mbalimbali nchini na kukamata jumla ya Kilo 34.89 za dawa za kulenya aina ya Heroin pamoja na watuhumiwa 11.

Amesema kuwa watuhumiwa waliokamatwa na dawa za kulevya aina ya heroine ni kocha wa makipa wa Simba, Muharami Sultan (40), mmiliki wa kituo cha Cambiasso Sport Academy kilichopo Tuangoma, Kambi Zuberi Seif (40). Pia wamo Said Matwiko mkazi Magole (41), Maulid Mzungu maarufu Mbonde (54) mkazi wa kisemvule ambaye ni ndugu na kocha wa makipa wa Simba Muharami.

Wengine ni John John maarufu Chipanda (40) ambaye jukumu lake kutafuta vijana wenye vipaji na kuwapeleka Cambiasso Sport Academy

Hata hivyo Mamlaka hiyo imewakumbusha wananchi kuwa kujihusisha kwa namna yeyeote na dawa za kulevya ni kosa kisheria kwani Sheria ya kudhibiti na kupambana na dawa za Kulevya (sura ya 95) inatoa adhabu kali hadi kifungo cha maisha kwa atakayethibitika kujihusisha na kosa hilo.

0/Post a Comment/Comments