Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Dkt. Oswald Masebo akifungua Mkutano wa Nane wa Baraza la Wafanyakazi wa Makumbusho ya Taifa
Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Makumbusho ya Taifa akisikiliza kwa makini hotuba ya Mwenyekiti wa Bodi kwenye mkutano wa Baraza hilo
Baraza la Wafanyakazi wa Makumbusho ta Taifa wakiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Makumbusho ya Taifa baada ya kufungua mkutano wa Baraza
.........................
Na Mwandishi Wetu
Watumishi wa Makumbusho ya Taifa wametakiwa kuhamasisha jamii ili kuthamini na kuenzi mchango wa Makumbusho ya Taifa katika kujenga na kuhifadhi historia ya nchi ya Tanzania.
Hayo yamesemwa na Mwenyekti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Oswald Masebo wakati akifungua Baraza la Nane la Wafanyakazi wa Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam.
Dkt. Masebo amesema kwa sehemu kubwa jamii haijatambua umuhimu wa Makumbusho ya Taifa ambayo inashughulikia urithi wa utamaduni na historia ya nchi inayounda nguvu laini ya Taifa la Tanzania.
“Makumbusho ya Taifa inatunza na kulinda misingi ya utamaduni wetu, historia yetu, utaifa wetu, uzalendo wetu, na utu wetu” amesema Dkt. Masebo na kuongeza kuwa mambo yanayosimamiwa na Makumbusho ya Taifa yanayounda nguvu laini ya Taifa la Tanzania.
Dkt. Masebo amewataka wajumbe wa Baraza hilo kutoa elimu na kuhamasisha jamii ili waweze kutambua umuhimu wa Makumbusho ya Taifa katika kujenga nchi yenye maadili na mshikamano.
“Jamii ikiwa na uelewa sahihi juu ya Makumbusho ya Taifa, watu watajenga shauku kubwa kutembelea Makumbusho, kufanya utalii wa ndani katika makumbusho, na kuiona Makumbusho kama taasisi muhimu kwa ustawi na usalama wa taifa letu” amesema Dkt Masebo.
Ameipongeza Menejimenti ya Makumbusho ya Taifa pamoja na Baraza la Wafanyakazi kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wakiifanya ya kuhifadhi urithi wa asili na utamaduni wa nchi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Makumbusho ya Taifa amesema Baraza la wafanyakazi ni chombo muhimu katika kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Taasisi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa. Dkt Noel Lwoga amesema kuwa Baraza la Wafanyakazi kwa kushirikiana na Menejimenti wameweza kutekeleza majukumu ya Taasisi kwa kufuata sheria na kanuni.
Post a Comment