Mamlaka
ya Hali ya Hewa Tanzania -TMA imesema ongezeko la joto katika baadhi ya maeneo
nchini imesababishwa na kusogea kwa jua
la utosi sambamba na upungufu wa mvua katika maeneo mengi kama ilivyotabiriwa
na Mamlaka hiyo.
Pia imesema Jua la utosi huambatana na hali ya ongezeko la joto kwa sababu uso wa dunia katika eneo tajwa huwa karibu zaidi na jua kuliko maeneo mengine.
Imeelezwa kuwa pia kwa kawaida vipindi vya jua la utosi nchini hufikia kilele mwishoni mwa mwezi Novemba wakati jua la utosi likiwa linaelekea kusini (Tropiki ya Kaprikoni) na hali hiyo hujirudia tena mwezi Februari wakati jua la utosi likiwa linaelekea kaskazini (Tropiki ya Kansa).
Hayo
yameelezwa jijini Dar es salaam na Mtaalamu wa Hali ya hewa TMA Joyce Makwata
ambapo amesema kuwa katika wiki mbili za mwanzo za mwezi Novemba, mwaka huu
hali ya ongezeko la joto imeendelea kujitokeza katika baadhi ya maeneo ambapo
kituo cha Mpanda kiliripoti nyuzi joto 35.4 0C ikiwa ni ongezeko la
nyuzi joto 4.7 ukilinganisha na wastani wa muda mrefu kwa mwezi Novemba na katika
kituo cha Tabora kiliripoti nyuzi joto 34.8 (ongezeko la nyuzi joto 3.7).
‘ katika wiki mbili za mwanzo za mwezi Novemba, 2022; hali ya ongezeko la joto iliendelea kujitokeza katika baadhi ya maeneo ambapo kituo cha Mpanda kiliripoti nyuzi joto 35.4 0C mnamo tarehe 2 Novemba, 2022 ikiwa ni ongezeko la nyuzi joto 4.7 ukilinganisha na wastani wa muda mrefu kwa mwezi Novemba. Kituo cha Tabora kiliripoti nyuzi joto 34.8 (ongezeko la nyuzi joto 3.7), Dar es Salaam nyuzi joto 33.7 (ongezeko la nyuzi joto 2.1) pamoja na Kilimanjaro nyuzi joto 34.3 (ongezeko la nyuzi joto 2.4)’ameeleza Makwata
Aidha
amesema kuwa vipindi vya ongezeko la joto vinatarajiwa kuendelea kujitokeza
katika mwezi Novemba, 2022 hususan katika maeneo yanayotarajiwa kuendelea kuwa
na upungufu wa mvua na kupungua kidogo ifikapo mwezi Disemba, 2022 ambapo
ongezeko la mtawanyiko wa mvua unatarajiwa.
Mamlaka Hiyo imetoa wito kwa wananchi kufuatilia taarifa za mwenendo wa hali ya hewa zinazotolewa pamoja na kutafuta, kupata na kutumia ushauri wa wataalamu wa kisekta ili kuepuka au kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na hali mbaya ya hewa ikiwemo ongezeko la joto.

Post a Comment