Xxxxxxxxxxxxx
Na Daniel Limbe,Kahama
Zaidi ya wananchi 300 kwenye kijiji cha Kakola wilayani Kahama mkoani shinyanga,wamemwomba rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati mgogoro wa ardhi uliodumu zaidi ya miaka 20 kati yao na mgodi wa Barrick Gold Corporation.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku chache baada ya Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa, kuwataka walalamikaji wa fidia kwenye mgodi wa North Mara kujitokeza wakiwa na nyaraka sahihi ili kuhakikiwa wanao stahili kulipwa.
Kutokana na kauli hiyo,baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kakola wameibuka na kumwomba rais Samia kuwasaidia kupata fidia ya maeneo yao,ambayo awali waliyamiliki na kuyaendeleza kabla ya ujio wa kampuni ya madini ya Bulyanhuru gold Mine ,Acacia na hatimaye Barrick.
Emmamuel Bombeda, amesema wamefikia hatua hiyo baada ya kutafuta haki yao kwa zaidi ya miaka 20 pasipo mafanikio hatua ambayo imesababisha wengine kati yao kufariki dunia pasipo kujua hatma ya fidia zao.
"Kitendo cha serikali kutuondoa kwa nguvu kwenye maeneo yetu kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita kisha ardhi yetu kuendelezwa na mgodi wa Barrick kwa shughuli za uchimbaji pasipo kutulipa fidia kumesababisha wananchi 363 kuwa maskini wa kutupwa na hata wengine wamekufa pasipo kupata hata jasho lao" amesema Emmanuel
Idadi hiyo inahusisha makundi ya aina tatu wakiwemo,wamiliki wa mashamba,wachimbaji wadogo na baadhi ya wafanyakazi wa mgodi huo walioumia wakiwa kazini na kuachishwa kazi mwaka 2007 kwa nyakati tofauti pasipo kupewa stahiki zao.
Naye George Kingi,ambaye ni miongoni mwa wadai wa fidia, amesema kabla ya kuondolewa, maeneo hayo yalikuwa na nyumba za kuishi,mazao na mashimo ya wachimbaji wadogo ambao pia waliondolewa kwa amri ya serikali mwaka 1996.
"Tumemwona rais wetu alivyo mpenda haki na mwenye huruma na watanzania...juzi ametangaza kuwalipa mafao yatokanayo na michango ya mifuko ya jamii watumishi wa vyeti feki...tunaamini hata sisi mgogoro huu ukimfikia ataguswa na kuhakikisha nasi tunapewa haki yetu ambayo imeminywa na watu wachache kwa maslahi yao binafsi"amesema Kingi.
"Kwa kipindi chote hicho tumefuatilia haki zetu ikiwa ni pamoja na kutafuta namna ya kuonana na rais watatu waliopita pasipo mafanikio...kwa hivyo tunaamini nafasi yetu ya mwisho ipo mikononi mwa rais Samia iwapo ujumbe wetu utamfikia" amesema.
Licha ya aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Msalala, Bhikhu Mohamed,kuwasilisha hoja ya mgogoro huo kwenye vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania julai 26 mwaka 1996 bado wananchi hao hawakulipwa(Nakala ya hotuba hiyo tunayo).
Alipotakiwa kuzungumzia malalamiko hayo, Ofisa uhusiano wa mgodi wa Barrick,Agapiti Kisoka,amesema hana muda mrefu tangu amekuwa kwenye ofisi hiyo na kwamba baadhi ya madai ya wananchi hayajui huku akidai anachoelewa ni kwamba mgodi unapotaka kuongeza eneo hufanya makubaliano na wananchi kwaajili ya kuwalipa fidia.
Kwa upande wake, Ofisa madini wilaya ya Kahama mkoani shinyanga, Emmanuel Hango, amethibitisha kuwepo kwa malalamiko yanayohusu fidia za wananchi na kwamba suala hilo bado linaendelea kushughulikiwa na mamlaka za serikali.
Mkuu wa wilaya ya Kahama,Festo Kiswaga,alipotafutwa kwa njia ya simu ili kuzungumzia malalamiko hayo pamoja na hatua iliyofikiwa kwaajili ya fidia,simu yake iliita pasipo kupokelewa kwa zaidi ya siku tatu.
Mwisho.

Post a Comment