WATU 700,000 DUNIANI KOTE HUFARIKI KILA MWAKA KUTOKANA NA USUGU WA VIMELEA DHIDI YA DAWA

Mfamasia kutoka shirika la Afya Duniani -WHO, Rose Shija akizungumza Jijini Dar es salaam katika kongamano la siku mbili

Mganga mkuu wa serikali Profesa Tumaini Nagu akizungumza Jijini Dar es salaam katika kongamano la siku mbili Novemba 22 - 23.


Profesa Hezron Nonga, Mganga mkuu wa wanyama Tanzania akizungumza Jijini Dar es salaam katika uzinduzi wa kongamano la kuhamasisha matumizi bora ya dawa

.........................

Na: Issa Mohamed –Dar es salaam

Email: issamohamed765@gmail.com

Takribani watu laki saba hupoteza maisha kila mwaka Duniani kote kutokana na madhara ya usugu wa vimelea dhidi ya dawa za antibayotiki huku vifo hivyo vikitarajiwa kuongeza hadi kufikia milioni kumi ifikapo mwaka 2050 endapo hatua sahihi zisipochukuliwa.

Mganga mkuu wa serikali Profesa Tumaini Nagu ameyasema hayo Jijini Dar es salaam wakati akifungua kongamano la siku mbili ambalo limelenga kuhamasisha matumizi bora ya dawa pamoja na kuongeza ufahamu wa madhara dhidi ya matumizi holela ya dawa za antibayotiki.

Profesa Nagu amesema nchini Tanzania usugu wa vimelea imefikia asilimia 60 huku miongoni mwa sababu zinazosababisha usugu huo ni pamoja na kutotumia dawa kwa usahihi.

‘’Vimelea hivi vinaweza kujenga usugu kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutotumia dawa kwa usahihi kwamfano kutumia dawa chini ya maelekezo ya daktari, sababu nyinginine ni matumizi ya dawa kabla ya kupima’’ Amebainisha Profesa Nagu.

Profesa Hezron Nonga ni mganga mkuu wa wanyama Nchini Tanzania amesema serikali kupitia kamati hiyo imekamilisha mapitio ya Mpango wa Kitaifa wa mapambano Dhidi ya Usugu wa Dawa wa 2017-2022 na imetayarisha mpango mpya wa 2023-2028, ambao unatarajiwa kuzinduliwa wakati wa wiki ya mapambano dhidi ya usugu wa dawa.

‘’Kuna mifugo tunatumia kama chakula na mingine hutumika kwa shughuli mbalimbali kama vile ulinzi, hivyo wafugaji hawapaswi kuwatibu wanyama hao isipkua ni Daktari pekee’’ Amesema Profesa Nonga.

Kwa upande wake mfamasia kutoka shirika la afya Duniani –WHO, Rose Shija amesema kwa mwaka 2019 pekee vifo milioni 4.95 vilihusishwa  kutokana na maambukizi ya bakteria wenye usugu dhidi ya dawa.

Kongamano hilo limewakutanisha wizara ya Afya, Wizara ya mifugo na uvuvi na wizara ya kilimo kupitia kamati ya kitaifa ya kuratibu shughuli za kuzuia usugu wa vijidudu dhidi ya dawa baridi kwa kushirikiana na mradi wa –HPSS tuhimarishe afya, vyuo vikuu na taasisi za utafiti.


 

0/Post a Comment/Comments