***
Kampuni ya CFAO Motors Tanzania ambao ni wasambazaji wakubwa wa magari Tanzania imepanua wigo kwa kufungua duka la kuuza vipuri halisi na vyenye ubora wa juu vya magari. Duka hilo linalofahamika kama WinPart limezinduliwa rasmi Novemba 11, 2022 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya CFAO Motors Tanzania, Fransois Bompart amesema uamuzi wa kufungua duka la vipuri halisi na vilivyo na ubora mkubwa kwenye soko la Tanzania umetokana na matatizo sugu wanayokumbana nayo wamiliki wa magari na mafundi wa magari kwa kuuziwa vipuri feki na visivyokidhi ubora.
Bompart amesisitiza kwamba WinPart inauza vipuri ambavyo vimethibitishwa kimataifa na ambavyo vinaingizwa nchini kutoka kwa watengenezaji wa vifaa halisi vya magari.
“Kwa kuzingatia changamoto wanazokumbana nazo wamiliki wa magari, mafundi wa magari, na watoa huduma za magari kutokana na kukithiri kwa uuzaji wa vipuri visivyokidhi ubora, tunayo furaha kuitambulisha Winpart ambayo iko chini ya kampuni ya CFAO Motors Tanzania. WinPart ni muuzaji mpya wa vipuri vya magari inayosambaza vipuri vya ubora wa juu vilivyoidhinishwa moja kwa moja kutoka kwa watengenezaji wa vifaa halisi kama vile Denso, Kavo, Valeo, Lumileds, Mann, Almabat, Riken, Techking na Pirelli”, amesema Bompart.
Kwa upande mwingine, Munir Ladak, Meneja wa Huduma wa CFAO Motors Tanzania alisema duka hilo ni kwa ajili ya kila mmoja aliye katika sekta ya magari kuanzia wauzaji wa jumla wa vipuri, mafundi wa mgari na wamiliki wa magari. Ladak amesema mbali na vipuri hivyo kuwa halisi na vyenye ubora mkubwa, bei zake pia zitazingatia uhalisia wa uchumi wa Watanzania.
“WinPart ni mkombozi kwa wamiliki wa magari. Kupitia vipuri halisi vilivyothibitishwa na watengenezaji wa vipuri vya magari duniani, wamiliki wa magari wana uhakika wa kuhakikisha magari yao yanadumu kwa muda uliotarajiwa. Jambo lingine kubwa ni kwamba Winpart tunazingatia uhalisia wa uwezo wa Tanzania kununua vipuri vya magari kwa kuweka bei zenye uhalisia na rafiki kwa makundi yote yanayokusudiwa kunufaika na vifaa vyetu”, amesema Ladak.
Duka la WinPart lipo Kariakoo - Mtaa wa Msimbazi jijini Dar es salaam, na linasambaza vipuri vya ubora wa hali ya juu kwa wauzaji wa jumla, maduka ya vipuri, pamoja na wateja ambao ni mmiliki mmoja mmoja wa magari.
Tanzania ni moja ya nchi ambayo huingiza kiwango kikubwa cha magari ambayo yameshatumika katika masoko mengine hivyo ni muhimu zaidi kuwa na mauzo ya vipuri vya magari vinavyokidhi ubora ili kuhakikisha magari yanadumu kwa muda mrefu na pia yanakuwa salama kwa watumiaji wa magari.
Post a Comment