Msafara wa timu ya waendesha baiskeli 50 kutoka Dar es Salaam umewasili katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwa lengo la kuhamasisha utalii wa ndani kuelekea msimu huu wa sikukuu.
Mratibu wa msafara huo unaojulikana kwa jina la “Pedal to Ngorongoro” Bw. Hillary Chuwa ameeleza kuwa msafara huo umeanzia eneo la Msasani Jijini Dar es Salaam na kuendesha baiskeli umbali wa takriban kilomita 785 kwa lengo la kuhamasisha utalii wa ndani katika vivutio vilivyopo eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
“Tumetumia siku 6 kutoka Dar es Salaam hadi Geti la Ngorongoro, lengo letu ni kutangaza utalii wa ndani na tumechangua Ngorongoro kama sehemu yenye maajabu mengi ya vivutio vya utalii, tunaamini kupitia kampeni yetu tuttaendelea kuitangaza na kuongeza idadi kubwa ya Utalii wa ndani” ameongeza Chuwa.
Timu hiyo iliyoanza kampeni ya utalii mwaka jana imetembelea Ngorongoro kwa mara ya pili na kuushukuru uongozi wa NCAA kwa kuwaunga mkono na kuimarisha uhusiano kupitia utalii wa baiskeli ulioongeza hamasha ya washiriki kutoka 30 mwaka jana hadi kufikia 50 mwaka huu na kuhusisha washiriki wa jinsia zote wengi wakiwa vijana.
Akipokea Ujumbe huo Naibu Kamishna wa Uhifadhi (Uhifadhi, Utalii na Maendeleo ya Jamii) Dkt. Christopher Timbuka amewashukuru waendesha baiskeli hao kwa kusafiri na baiskeli kutoka Dar es Salaam hadi Ngorongoro na kupeperusha bendera ya NCAA njia nzima.
Dkt. Timbuka amewahakikishia kuwa uongozi wa NCAA utaendelea kushirikiana timu hiyo katika kampeni ya kuhamasisha utalii wa ndani.
Akitoa maelezo ya msafara huo Msimamizi wa shughuli za Utalii NCAA Peter Makutian amewahakikishia kuwa Ngorongoro ni eneo lenye vivutio vingi vya utalii zikiwepo Kreta za Ngorongoro, Empakai na Olmoti.
Vivutio vingine ni pamoja na Makumbusho ya Olduvai, nyayo za Laetoli, Mchanga unaohama, eneo la tambarare za Ndutu maarufu kwa mazalia ya nyumbu na vivutio vingine vitakavyowawezesha waendesha baiskeli hao kuwa mabalozi wa Ngorongoro popote wanapokuwa.





Post a Comment