Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ameitaka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia hapa nchini kutoa kipaumbele cha juu zaidi katika kusaidia kukamilisha malipo ya majengo yanayotakiwa kununuliwa na Chuo Kikuu Huria Tanzania yaliopo eneo la Biafra Kinondoni Jijini Dar es salaam ili Chuo hicho kiweze kuwa na miundombinu ya kutosha.
Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 12 Desemba 2022 wakati alipotembelea Makao Makuu ya Chuo Kikuu Huria Tanzania yaliopo Kinondoni Jijini Dar es salaam. Amesema serikali itaendelea kuboresha mazingira ya chuo hicho ili kiweze kutoa elimu iliyo bora na hasa inayolenga kuwajengea wahitimu uwezo wa kujiajiri, kushindana katika soko la ajira, kuwa wabunifu na kushiriki katika fursa mbalimbali za kiuchumi.
Aidha ametoa wito kwa watafiti kujielekeza zaidi katika vipaumbele vya taifa ili kutatua changamoto mbalimbali. Makamu wa Rais amesema ni muhimu kuendeleza jitihada za vijana walioanzisha ubunifu unaotatua changamoto ikiwemo wale wanaotumia taka katika hatua za kutengeneza chakula cha mifugo na Samaki, wanaotengeza nishati mbadala pamoja na bidhaa za lishe zinazovutia Watoto hapa nchini.
Makamu wa Rais Dkt. Mpango ameutaka uongozi wa Chuo Kikuu Huria kukabiliana na wanafunzi wanaofanya udanganyifu katika uandishi wa tafiti zao ikiwemo kutumia watu wengine katika uandishi na kupata shahada mbalimbali. Amesema hali hiyo imeendelea kushusha hadhi ya Chuo Kikuu Huria pamoja na athari kubwa zimeendelea kuonekana katika soko la ajira ambapo wahitimu wanashindwa kukidhi mahitaji ya soko hilo. Ameongeza kwamba ili kufikia maendeleo ya haraka ni lazima kuwekeza kwenye ubora wa rasilimali watu ambao wanatokana elimu bora.
Awali akitembelea Mabanda ya maonesho katika Chuo hicho , Makamu wa Rais ametoa wito wa kwa vyuo hapa nchini kuzalisha wahitimu watakaoweza kuendana na sekta ya ajira ikiwemo mahitaji ya sekta binafsi. Pia ameiagiza Wizara ya Elimu , Sayansi na Teknolojia kuhakikisha vitendea kazi kwa ajili ya elimu ya Tehama kwa watu wenye mahitaji Maalum vinapatikana ili kuwasaidia kuweza kujifunza kirahisi. Aidha ameutaka uongozi wa chuo hicho kutangaza zaidi elimu inayotolewa katika chuo hicho ikiwemo Elimu adimu ya Anga na Nyota (Astronomy).
Kwa upande wake Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Adolph Mkenda amesema Chuo Kikuu Huria kimeendelea kutoa fursa ya kuwafikia watanzania wengi katika maeneo walipo ili waweze kuongeza elimu yao kwa kupitia elimu ya Masafa.
Pia Prof Mkenda amesema serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa elimu ya juu ikiwemo kuongeza kiwango cha mikopo kwa wanafunzi kutoka Bilioni 464 hadi kufikia bilioni 654. Aidha ameongeza kwamba wizara hiyo itasimamia utaoaji wa haki wa mikopo kwa kuzingatia zaidi wanafunzi wenye uhitaji mkubwa.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania, Profesa Elisaf Bisanda ameiomba serikali kusaidia gharama za mtandao ambazo hufikia bilioni 1 kwa mwaka kutokana na utoaji wa elimu ya Masafa. Pia ametaja changamoto zinazokabili chuo hicho zikiwemo za ukosefu wa majengo katika baadhi ya mikoa hapa nchini unaohitaji shilingi bilioni 4.5 katika ujenzi wake pamoja na upungufu wa vifaa vya tehama.
Post a Comment