Imebainishwa kuwa bado uelewa ni mdogo kwa jamii kuhusu athari zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi jambo ambalo linasababisha uwepo wa changamoto katika kuhakikisha kuwa mazingira yanalindwa ili kuepusha athari za ukame, uhaba wa maji na chakula na ongezeko la joto.
Hayo yameelezwa leo Jijini Dar es Salaam na Mratibu wa Gender Climate Change Coalition Tanzania Maria Matui katika hafla ya uzinduzi wa ripoti ya mabadiliko ya tabia nchi ambapo amesema mabadiliko hayo pia yanagusu haki za binadamu na makundi maalum ikiwemo watoto na kina mama.
“Kila eneo katika eneo la nchi linaathirika na mabadiliko ya tabia nchi na kuleta athari mbalimbali kwa jamii ikiwemo kukosekana kwa maji hivyo kuwapa wakati mgumu kinamama na watoto kutembea umbali mrefu kutafuta maji jambo ambalo husababisha wakumbane na changamoto nyingine za ukatili wa kijinsia “Amesema Bi Matui.
Aidha amesema uwepo wa sheria na kanuni zinazoendana sawa, ikiwemo sheria ya ardhi, sheria ya utalii na sheria ya kilimo zikifanya kazi sambamba zitawezesha kuepusha uharibifu wa mazingira na hifadhi asili ambazo hutunza mazingira hususani kufyonza hewa ya ukaa.
Hatahivyo amesema kuna haja ya elimu zaidi kutolewa kwa wananchi kuhusu sera na kanuni za kuingia kwenye biashara zinazo changia mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo zili za uchomaji mkaa upasuaji mbao ambazo kwa kiasi kikubwa huathiri mazingira.
Sambamba na hayo amesema ongezeko la uelewa kwa jamii kuhusu madhara ya mabadiliko ya Tabianchi, kutambua maeneo yanayoathirika kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya Tabianchi ikiwemo ukame ukosefu wa maji joto kali vitasaidia kupunguza shughuli zinazoathiri mazingira.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Youth Survival Organisation Hamphery Mrema amesema bado ushirikishwaji wa vijana ni mdogo katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya Tabianchi huku zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania ni umri chini ya miaka 35 ambao ni vijana na wakihusishwa kwenye masuala ya mabadiliko ya Tabianchi watakuwa na mchango mkubwa.
Aidha ameongeza kuwa kuna haja sasa kwa wadau mbalimbali wa utunzaji mazingira pamoja na serikali kuwapa kipaumbele vijana kwa kuwashirikisha toka hatua za awali ili kuwezesha ufanikishaji wa utunzaji wa mazingira kwa faida ya sasa na kizazi kijacho.

Post a Comment