Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema inaendelea kufuatilia kwa karibu changamoto ya mabadiliko ya Hali ya Hewa hususan ongezeko la joto na matukio ya hali mbaya ya Hewa ambayo yanaendelea kuathiri huduma katika sekta ya usafiri wa Anga na hivyo kuhitaji uimarishaji wa utoaji na matumizi ya taarifa za Hali ya Hewa.
Hayo yamejiri jijini Dodoma wakati Mamlaka hiyo imekutana na wadau wa usafiri wa Anga wa jijini Dodoma,ili kujadili maendeleo na mahitaji ya huduma za Hali ya Hewa kwa usafiri wa Anga.
Akifungua mkutano huo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu, TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a amesema kusudi la mkutano huo ni kutathimini maendeleo na mahitaji ya utoaji wa huduma za Hali ya Hewa kwa ajili ya usafiri wa Anga ili kuongeza tija na ufanisi katika shughuli na kuhakikisha usalama wa usafiri wa Anga.
Amesema kuwa TMA imeendelea kutambua umuhimu wa mikutano hiyo kwani imesaidia kuboresha sio tu ubora wa bidhaa zao bali pia taratibu za utoaji wa huduma katika sekta ya usafiri wa Anga.
“Nakumbuka, miaka ya nyuma kulikuwa na malalamiko kadhaa juu ya kutafuta njia bora ya kuhakikisha taarifa za Hali ya Hewa kwa marubani zinapatikana kwa njia ya mtandao yaani (online), TMA tulifanyia kazi malalamiko hayo na kuweza kutengeneza mfumo wa Tehama wa usambazaji wa taarifa hizo unaoitwa MAIS na kuanza kufanya kazi rasmi mwaka 2012.” Amesema Dkt. Ladislaus Chang’a.
Aidha Dkt. Chang’a amesisitiza kuwa TMA inafanya kazi kwa kuzingatia taratibu za Kitaifa na Kimataifa.
Akizungumzia kuhusu taratibu za Kimataifa, ameeleza kuwa TMA imeendelea kukaguliwa kila mwaka na kuendelea kushikilia cheti cha ubora na hivyo kuhakikishia ubora wa huduma zitolewazo kukidhi viwango vya Kimataifa.
Awali wakati akifungua Mkutano huo, aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuboresha miundo mbinu ya Hali ya Hewa kwa kufanya ununuzi wa vifaa mbalimbali vya kisasa vya hali ya hewa ikiwemo Rada.
.jpg)
Post a Comment