WAOMBA KUONANA NA RAIS SAMIA...NI BAADA YA KUDAI HAWANA IMANI NA DC KAHAMA




Xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxzx


Na Daniel Limbe,Kahama.

SIKU chache baada ya mkuu wa wilaya ya Kahama mkoni Shinyanga,Festo Kiswaga, kudai kuwa wananchi waliohamishwa kwa nguvu na serikali mwaka 1996 kwenye kijiji cha Kakola wilayani humo hawastahili kulipwa fidia yoyote, wananchi hao wamedai hawana imani na kiongozi huyo.

Kauli ya mkuu huyo wa wilaya ilimaanisha kuwa wananchi hao waliondolewa kipindi ambacho sheria iliyokuwa ikitumika ilikuwa haitoi haki kwa wananchi kulipwa fidia ya ardhi badala yake ilitambua maendelezo ya ardhi pekee.

Hata hivyo kauli hiyo,imepokelewa kwa hisia tofauti na baadhi ya waathirika wa maeneo yaliyotwaliwa kwa nguvu kisha kukabidhiwa mwekezaji wa mgodi wa Barrick Gold Mine, ambapo wamesema hawana imani naye kwa madai amekuwa akipindisha ukweli wa madai ya wananchi hao licha ya kuagizwa na viongozi wa juu kutatua changamoto hiyo.

"Tunavyohisi mkuu wa wilaya yetu ana maslahi na huu mgogoro maana ameshindwa kuutatua, hataki kutusikiliza walengwa badala yake ameegemea kulinda maslahi ya mwekezaji japo ukweli kamili anaujua" amesema Emmanuel Bombeda.

"Cha ajabu hata vikao vyetu vya kujadili namna ya kumfikia rais Samia Suluhu ili atusaidie kupata haki zetu navyo tumetupigwa marufuku na DC...hataki tukutane wala kujadili kuhusiana na dhuruma tuliyofanyiwa unategemea yeye kama kiongozi tutamuaminije...alihoji Bombeda.

Hata hivyo amedai maombi yao ni kwa rais Samia Suluhu Hassan,aweze kuingilia kati mgogoro huo ili wananchi hao wapate angalau kifuta jasho kutokana na walivyohangaika kuitunza na kuiendeleza ardhi hiyo kwa kupanda miti,kujenga nyumba, kuzika ndugu zao na hata kuilinda muda wote kabla ya kuporwa kwa nguvu na serikali.

Aliyekuwa kaimu mtendaji wa kijiji cha Kakola, George Kingi, ambaye pia ni mwathiliwa na mgogoro huo, anakiri maeneo ya wananchi hao yalitwaliwa kwa nguvu na serikali mwaka 1996 kwaajili ya uwekezaji wa mgodi wa dhahabu wa Barrick wilayani Kahama na kwamba hakuna mwananchi yeyote aliyelipwa maendelezo ya ardhi yake ispokuwa baadhi ya wachache waliogomea kuondoka eneo hilo ndiyo walipewa fidia mwaka 1997 na 1998.

"Mkuu wa wilaya anasema walioondolewa kwenye kijiji cha Kakola mwaka 1996 hawakuwa na haki ya kulipwa kwa sababu ya sheria iliyokuwepo kutowapa haki wananchi...je hao wachache wasiozidi 15 waliofanyiwa uthamini mwaka 1997 na 98 kisha kupewa fidia wao ilitumika sheria gani...?" alihoji Kingi.

Amesema kuwa mkuu wa wilaya hiyo,analenga kupotosha ukweli kutokana na maslahi yake binafsi na kwamba ili kuupata ukweli wa mambo wanaomba kukutana na rais Samia Suluhu ili awasikilize kilio chao ambacho kimedumu kwa zaidi ya miaka 25 pasipo kupata ufumbuzi.

"Tunaomba ieleweke kuwa sisi hatupingani na sheria iliyokuwepo ispokuwa tunachohitaji tupate angalau jasho letu...maana hata hiyo sheria ya kikoloni pamoja na mapungufu yake bado ilikuwa inatoa haki ya watu kulipwa maendelezo ya ardhi...basi tulipwe hata miti tuliyokuwa tumepanda,makazi yetu yaliyovunjwa na maskaveta pamoja na makaburi ya ndugu zetu tuliowazika hapo" amesema Kingi.

Hata hivyo mkuu wa wilaya hiyo,alidai iwapo kuna mwenye ushahidi unaoshikika kuwa anadai eneo lake aupeleke ofsini kwake ili hatua zaidi zichukuliwe.

Ofisa madini wilaya ya Kahama mkoani shinyanga,Emmanuel Hango, anakiri kuwepo kwa malalamiko ya baadhi ya wananchi kuhusiana na malipo ya fidia baada ya kuondolewa kwenye maeneo yao huku akidai kuwa taarifa zaidi zipo ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo.



Picha inaonyesha eneo ulipo mgodi wa Barrick Bulyanhulu Kakola.

             

Mkuu wa wilaya ya Kahama Festo Kiswaga
  Mwisho.

0/Post a Comment/Comments