AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MAISHA KWENDA JELA KWA KUMBAKA MTOTO WA MIAKA 3 NA MIEZI MIWILI

 

Xxxxxxxxxxxxxxxx

January 4th, 2023

Na Abel Paul wa Jeshi la Polisi 

Mahakama ya Wilaya ya Arumeru Mkoani Arusha imemhukumu kifungo cha maisha jera Bw. John Sanare Lukuaya  (23) mkazi wa Kijiji cha Kimnyaki, Kata ya Kimnyaki, halmasahuri ya Arusha kwa kosa la kumbaka mtoto wa miaka mitatu na miezi miwili ambaye inasadikika ni mtoto wa mke wake.

Akitoa hukumu hiyo leo Januari 04, 2023 Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya wilaya, Mheshimiwa Gwantwa Mwankunga,  amesema kuwa, Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha na ushahidi uliotolewa pasipo shaka yoyote na kumtia hatiani kwa kosa la kubaka.

Mwendesha mashitaka na Wakili wa Serikali Penina Ngotea, aliieleza mahakama hiyo kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo tarehe 10 Julai ,2022 katika Kijiji cha Kimnyaki ndani ya nyumba wanayoishi na mtoto huyo, ambapo alimbaka mtoto huyo wa miaka 3 na kumsababishia maumivu makali.

Muendesha mashtaka huyo, amefafanua kuwa, mtuhumiwa alimbaka mtoto huyo muda wa usiku,  wakati mama wa mtoto huyo akiwa amekwenda kulala kwenye msiba jirani huku mtuhumiwa akiwa amebaki na mtoto usiku huo.

Hivyo, aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mtuhumiwa kwa makosa hayo ili iwe ni fundisho kwa watu wengine wenye nia ya kutaka kufanya vitendo kama hivyo kwa watoto.

Upande huo wa mashitaka uliwasilisha mashahidi watano na mashahidi wanne walitoa ushahidi ambao pasipo na shaka yoyote mahakama ilimkuta mtuhumiwa na kosa hilo, na kuamua kumtia hatiani kufungwa kifungo cha maisha kwa kosa la kubaka.

Awali mkurugenzi wa shirika la CWCD Hindu Mbwega, ameishukuru mahakama kwa kumtia hatiani mtuhumiwa huyo, kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ukatili kwa watoto, na kuionya jamii kufichua vitendo vya ukatili vinayofanyiwa watoto na kuwataka kutambua kuwa sheria inafanya kazi kwa yeyote atakayejihusisha na vitendo hivyo.

Naye Afisa Ustawi wa Jamii, halmashauri ya Arusha, Beatrice Tengi ameipongeza mahakama kwa kutenda haki kwa kuhakikisha haki ya mtoto imepatikana

Ameongeza kuwa licha ya kuwa serikali kwa kushirikiana na wadau inatoa elimu kwa kwa jamii juu haki za watoto, bado kuna changamoto kwa jamii kufanya ukatili kwa watoto na baadhi ya wanajamii kushindwa kutoa ushahidi kwenye kesi kwa kuhofia kutengwa na ndugu, jamaa na marafiki.

0/Post a Comment/Comments