Kwa mara nyingine, uovu mwingine, kumwagiwa vumbi juu ya jua
Vibaraka na mamluki wa shetani, kila mara huvunjia heshima matukufu ya Kiislamu kwa visingizio visivyo na maana, huku wakipata himaya na uungaji mkono wa madola yanayojidai kuwa ni wafuasi na watetezi wa uhuru wa kusema.
Mara hii tumeshuhudia kuchomwa moto nyoyo na roho za mamilioni ya Waislamu; yaani Qur’ani Tukufu, kitendo ambacho kilifanywa mbele ya ubalozi wa Uturuki katika mji mkuu wa Sweden Stockholm. Hii sio mara ya kwanza kuona nchi ya Sweden ikifanywa kuwa uwanja ya maonyesho ya kishetani dhidi ya Uislamu na Waislamu.
Waislamu wanapata uhai kupitia Qur’ani Tukufu na hivyo kuelekea kwa Mwenyezi Mungu. Qur’ani Tukufu Kwa Waislamu ni kitabu cha uhai, kifo na ufufuo.
Waislamu husoma Aya za kitabu hiki cha Mwenyezi Mungu usiku na mchana, humuomba dua Mwenyezi Mungu kwa Qur’ani na wanakitukuza na kukiheshimu kitabu hiki huku wakiwa na mapenzi makubwa nacho, na wana mfungano na kitabu hiki cha mbinguni katika kipindi cha maisha yao ardhini.
Kufanywa maonyesho kama haya ya kidhalili (kuchoma nakala ya Qur’ani) kwa kisingizio cha kulinda uhuru wa kusema ni kitendo cha kikatili na dhulma isiyo na mwisho dhidi ya Waislamu ambao wenyewe daima wanaheshimu matukufu, nembo, athari na maeneo ya ibada ya dini za wengine.
Ni kwa msingi huo ndio maana maonyesho kama haya yanazusha hasira na ghadhabu.
Hapana shaka kuwa, vitendo viovu na vya kishari kama hivi vinatoa pigo kubwa kwa suala la kuishi kwa amani na usalama baina ya wafuasi wa dini mbalimbali, itikadi na tamaduni na wakati huo huo, vinatia dosari anga ya mazungumzo na ushirikiano baina ya watu wa tamaduni tofauti.
Mimi nikiwa Mkuu wa Baraza la Uandaaji Sera na Uratibu wa Mazungumzo ya Dini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ninalaani vikali kuchomwa moto Qur’ani Tukufu, kutusiwa na kuvunjiwa heshima matukufu ya kidini na kujeruhiwa nyoyo za mamilioni ya Waislamu.
Kwa akali wafuasi wa Qur’ani Tukufu wanataraji kuwaona viongozi wa dini, wanafikra na watu huru duniani hususan wakazi wa Ulaya Magharibi na Amerika ya Kaskazini ambao kwa miaka mingi wameona maeneo hayo yakibadilishwa na kuwa uwanja wa maonyesho haya ya kifedheha wakitangaza kujibari na kujiweka mbali kwa uwazi kabisa na chuki hizi dhidi ya Uislamu na kuumizwa nyoyo za Waislamu na hivyo kufichua mpango wa uongo na bandia wa kufungamanisha uhuru wa kusema na kuvunjia heshima matukufu ya kidini.
Ninamuomba Mwenyezi Mtukufu asituweke mbali na huruma, nuru na njia Yake.
Mohammad Mahdi Imanipour
Mkuu wa Baraza la Uandaaji Sera na Uratibu wa Mazungumzo ya Dini
Jamadithani 1444 Hijria
Januari 2023

Post a Comment