Wanafunzi wakisikiliza kwa makini maelekezo kutoka kwa Waziri wa Tamisemi,Angellah Kairuki.
Waziri wa Tamisemi,Angellah Kairuki akizungumza na wanafunzi wa kidato cha kwanza shule ya sekondari Sofu.
WANAFUNZI nchini wameagizwa kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia mashuleni ili hatua za kisheria zichukuliwe haraka badala ya kuficha na kuishi na msongo wa mawazo.
Hatua hiyo itasaidia kupunguza wimbi la ukatili huo mashuleni na kwenye jamii wanazoishi watoto hao, kwa lengo la kuwa na jamii yenye ustawi bora kwa maendeleo ya nchi.
Hayo yamesemwa leo na waziri wa nchi Ofisi ya rais Tamisemi, Angellah Kairuki, alipotembelea shule ya sekondari Sofu iliyopo Kibaha mkoani Pwani kisha kuzungumza na walimu na wanafunzi waliojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2023.
"Ninawasihi msome sana na ukiona kwa namna yoyote mtu anakushinikiza kuacha masomo, au unafanyiwa ukatili majumbani au kuna mwalimu hapa anakufanyia ukatili wa kimwili,ki jinsia, ki akili,ki saikolijia au kingono toa taarifa kwa mkuu wa shule...pia ninaamini walimu mtakuwa mmeshawapitisha kwenye elimu hiyo kabla ya kuanza masomo" amesema Kairuki.
"Na ikitokea ukaona hujapata msaada hapa shuleni ulizia taratibu zilipo ofisi za mkuu wa wilaya...ukiulizwa unamtaka wa nini waambie kuna mzazi wangu anataka kuongea naye...serikali yenu ipo imara na itaendelea kuwalinda ili msome hadi vyuo vikuu".
Kadhalika ametumia fursa hiyo, kuiasa jamii kujikita kwenye ujenzi wa shule za ghorofa badala ya ujenzi wa kutawanya majengo ambao umekuwa ukitumia eneo kubwa.
Hatua hiyo imekuja baada ya diwani wa kata ya Sofu ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya mji Kibaha,Mussa Ndomba,kumweleza waziri kuwa wilaya hiyo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa maeneo ya ujenzi wa shule na huduma za afya, jambo ambalo serikali inapaswa kusaidia upatikanaji wa maeneo hayo kutoka kwa baadhi ya mashirika ikiwemo lile la elimu Kibaha.
Mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge,akawataka wazazi kundelea kufuatilia maendeleo ya watoto wao majumbani ikiwa ni pamoja na kukagua madaftari ya wanafunzi hao badala ya kuwaachia kazi hiyo walimu.
"Niwatake wazazi kufuatilia maendeleo ya masomo ya watoto wao...wewe hata kama hujui kusoma unashindwaje kujua hii ni kosa na hii vema...alihoji Kunenge.
Ofisa elimu sekondari,halmashauri ya mji Kibaha, Rosemary Msaki, mbali na kuipongeza serikali kwa jitihada kubwa za ujenzi wa miundo mbinu ya shule kwenye kata hiyo,amesema awali wanafunzi hao walikuwa wakitembea umbari mrefu kwenda sekondari ya Pangani,Picha ya ndege na nyumbu jambo lililokuwa likisababisha kuota vigimbi kwenye miguu yao.
Mwisho.




Post a Comment