Wito umetolewa kwa Watanzania kujifunza kuwekeza kwenye afya zao kwa kujiunga na skimu mbalimbali za bima ya afya ili kumudu gharama za matibabu.
Wito huo umetolewa an Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo mara baada ya kutembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili - Mloganzila na kuzungumza na wananchi waliofika Hospitalini hapo kupata huduma za matibabu, kuona hali ya utoaji huduma za afya pamoja na kuzungumza na watumishi wa afya.
“Ni lazima Watanzania watambue kwamba bila afya bora hakuna maisha, afya ndio kila kitu, bila afya bora huwezi kufanya kazi au shughuli yeyote ya kiuchumi, ni lazima waanze kuwekeza kwenye afya zao” amesema Waziri Ummy Mwalimu
Waziri Ummy amekemea tabia ya watu wanaoomba misahama katika Vituo vya umma vya kutolea huduma za afya huku wakiwa wamepewa rufaa kutoka Hospitali binafsi ambapo wamelipa gharama kubwa za matibabu.
“Mgonjwa anaanzia ‘Private’ akishakuwa hoi ndio wanamkimbika katika Hospitali ya umma tunahangaika naye, mgonjwa huyo huyo ameenda ‘Private’ analipa fedha zote, wakiishiwa wanakuja Serikalini huku wanaomba msamaha hawana uwezo”
Waziri Ummy amesema kuwa hakatazi wagonjwa kwenda katika Vituo binafsi lakini wanapokwenda huko ni lazima wafanye maamuzi sahihi huku akisema kuwa hata wakija katika Vituo vya Umma watalazimika kuliipia gharama hivyo hivyo.

Post a Comment