MWENYEKITI wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi(UWT) Mkoa wa Njombe Scolastika Kevela amelaaini vikali tukio la mauaji binti wa miaka 17 Eliza Mlimbila lililotokea Mji wa Makambako mkoani humo na kulitaka Jeshi la Polisi kuchukua hatua za haraka kuwakamata wahusika.
Akizungumza leo, Kevela ambaye ni mjumbe wa Mkutano Kuu ya CCM Taifa, amesema kitendo kilichofanywa na watu hao kamwe hakiwezi kufumbiwa macho na ni ukiukwaji wa haki za binadamu na kusisitiza kwa vyovyote waliohusika wamakatwe kwa ajili ya sheria kuchukua mkondo wake.
Marehemu Eliza Mlimbila mkazi wa mtaa Sigridi uliopo kata ya Kivavi halmashauri ya mji wa Makambako mkoani Njombe alikutwa amefariki katika mtaa wa Kahawa mjini humo huku chanzo cha kifo chake ikitajwa kuwa ni kutokana na kubakwa,kulawitiwa na kukabwa shingo siku ya mkesha wa mwaka mpya.
" UWT Mkoa wa Njombe tunalaani vikali tukio hili la kinyama lililofanywa kwa binti huyo mdogo ambaye bado alikuwa na ndoto zake za kimaisha, tunaviomba vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua za haraka kuwabaini waharifu na kuwachukulia hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa watu wenye tabia hizo" amesema Kevela
Amesema wao kama Umoja wa Wanawake wa Mkoa wa Njombe wamehuzunishwa na kitendo hicho kilichofanywa kwa binti huyo mhitimu wa kidato cha nne mwaka 2022 huku akitoa pole kwa wazazi na wafiwa wote na kuitaka jamii ya wana Makambako kutoa ushirikiano kwa vyombo vya usalama ili wahusika waweze kukamatwa.
Awali Baba mzazi wa binti huyo Meshack Mlimbila amesema mtoto wake alichelewa kurudi nyumbani siku ya jumamosi ya Disember 31 na alipoulizwa alikuwa wapi aliondoka tena bila kuaga mpaka alipopata taarifa za kifo chake siku ya mwaka mpya
“Jumamosi tumetoka shambani hatukumkuta nyubani mpaka saa tatu aliporudi nikamuuliza lakini alivyotoka toka sikuelewa tena na kwa sababu alikuwa anaweza kutoka na kurudi kwa hiyo mpaka mauti inamkuta sielewi alikuwa wapi,mara kadhaa tumemuonya lakini sijui ni kwa nini haya magenge yake kwasabu unaweza ukamwambia akakuelewa halafu ukakuta tena hayupo”amesema Mlimbila
Kwenye mazishi ya Eliza yaliyofanyika katika makaburi ya Magegere Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Njombe ambaye ni mbunge wa jimbo la Makambako Deo Sanga ameagiza jeshi la polisi kuhakikisha linawakamata wote ambao wamehusika na tukio hilo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe Hamis Issah amehudhuria katika mazishi ya binti huyo na kuwahakikishia wananchi kuwa wahusika wote watakamatwa huku akiomba waendelee kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu kwao wakati polisi wakiendelea na uchunguzi.
“Binti amezaliwa mwaka 2005 halafu anafariki kwa kusababishiwa na mtu haiwezekani,sisi tutafuata taratibu zote kuhakikisha jambo hili tunalishughulikia na wanamakambako muwe na imani jambo la msingi niwaombe tuwe na ushirikiano”amesema Kamanda Issah
Ends
Post a Comment