WACHIMBAJI WA MGODI WA IGALULA WAIANGUKIA SERIKALI UMEME

Mkurugenzi mtendaji wa mgodi wa Igalula Husein Makubi akiwa ameishikilia jiwe lenye kusadikika kuwa na madini ya dhahabu mgodini hapo

Mkurugenzi mtendaji wa mgodi wa Igalula Husein Makubi wa kwanza kushoto akiwa na mameneja wa mgodi uho wakati wakiongea na waandishi wa habari waliofika mgodini hapo

....,......,......

 Na Richard Mrusha 

MKURUGENZI Mtendaji wa Mgodi wa Igalula uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale Mkoani Geita Hussein Makubi maarufu Mwananyanzara, ameiomba serikali kupitia Wizara ya Nishati kuweza kuwaletea Umeme katika Mgodi huo ili kuweza kuleta tija ya uzalishaji wa Madini ya Dhahabu.

Kwani kwa kukosekana miundombinu ya umeme katika Mgodi huo kunapelekea kushuka kwa uzalishaji wa Madini hayo kwani gharama za mafuta yanayotumika kuendeshea mitambo ya uzalishaji ni kubwa ukilinganisha na kupanda kwa nishati ya mafuta hayo.

Mkurugenzi huyo amesema kuwa kupatikana kwa nishati hiyo kutaongeza tija kwani Wachimbaji wadogo watazalisha zaidi kuliko hivi sasa, maana wanalazimika kutumia Nishati mbadala ya mafuta kutokana na kukosekana kwa Nishati ya umeme.

Mwananyanzara ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa mgodi huo wenye takribani ya watu zaidi ya 6,000 ameyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari waliotembelea mgodi huo kwa lengo la kujionea shughuli zinazoendelea kufanyika katika Mgodi huo.

Amesema kuwa kuna umuhimu wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuona umuhimu wa kuwezesha wachimbaji wadogo katika maeneo ya migodi hasa kwa upande wa miundombinu bora ya Maji safi na salama, Umeme pamoja na barabara ili kurahisisha uendeshaji wa shughuli hizo

Pamoja na Mambo mengine Mwananyanzara amempongeza Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko kwa hatua ya kuweza kusimamia vizuri sekta hiyo na kupunguza tozo mbalimbali ambazo zimefanya wachimbaji kupata nguvu ya kuendelea na shughuli zao na kupata kipato kinachoweza kuendesha Maisha yao.

 Akizungumzia upande wa utunzaji wa mazingira Mwananyanzara amesema kuwa yapo maeneo ambayo ni maalumu kwa shughuli za uchimbaji lakini pia kuna maeneo ndani ya mgodi yameandaliwa kwaajili ya upandaji wa miti ili kurejesha uoto wa asili.

Hata hivyo kwa upande wake meneja wa mgodi huo Chuma Sayi amesema walianza shughuli za Uchimbaji wa Madini ya Dhahabu katika eneo hilo kipindi cha mwaka 2019 mwezi wa nne ambapo hadi sasa shughuli za uchimbaji zinaendelea huku akieleza kuwa Mgodi unaendelea kushirikiana na jamii pamoja na serikali ya Kijiji kwa shughuli  za maendeleo ya Kijiji ikiwemo ujenzi wa shule na Zahanati ya Kijiji hicho.

“Ndugu waandishi wa Habari tunaendelea kushirikiana na jamii pamoja na Kijiji kwa shughuli za maendeleo mfano serikali ya Kijiji cha Kayenze tumeshirikiana nayo kujenga Zahanati ambayo mpaka sasa inatumika kuhudumia wananchi pamoja na Ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa ya shule ya Sekondari ambayo nayo mpaka sasa wanafunzi wanasoma hii yote ni ushiriki wa Mgodi,” amesema Chuma Sayi meneja wa Mgodi wa Igalula.

Meneja huyo wa Mgodi amesema kuwa suala la usalama ndani ya mgodi ni kubwa hivyo hakuna historia ya vifo  na kuongeza kuwa uongozi wa Mgodi huo una mahusiano mazuri na wafanyakazi  ambapo  shughuli za uchimbaji zinafanyika kwa amani bila bughuza yoyote ile kwa vile wakileta changamoto zao zinatatuliwa haraka.

Naye mchimbaji Lambeli bert ameupongeza mgodi huo kwa ushirikiano unaowapatia wachimbaji hao hasa kupitia idara ya ukaguzi wa mgodi jambo ambalo limepelekea mgodi huo kukosa matukio ya vifo na kuongeza kuwa kitendo cha kuisaidia jamii inayozunguka mgodi huo kinafanya mgodi usemwe vizuri.

0/Post a Comment/Comments