Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya Chato wakiendelea kusikiliza hoja mbalimbali
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na Daniel Limbe,Chato
MKUU wa wilaya ya Chato mkoani Geita, Deusdedith Katwale,amekemea ukosefu wa uzalendo na uwajibikaji mbovu wa baadhi ya watumishi wa serikali wilayani humo huku akiwataka kubadilika katika uwajibikaji wao.
Aidha amedai hatoweza kubadili msimamo wake katika kusimamia haki za wananchi kwa maslahi mapana ya jamii na kwamba hatokuwa tayali kulinda watu wachache wenye lengo la kujipatia maslahi binafsi.
Ametoa kauli hiyo leo kwenye kikao cha Baraza la madiwani wa halmashauri ya Chato,huku akitoa mfano wa baadhi ya watumishi wachache aliowagusa na baadaye akaanza kupokea simu nyingi zenye lengo la kumkatisha tamaa kwa jitihada zake za kusimamia maslahi ya umma.
"Naomba niwathibitishie kuwa sitayumbishwa na yoyote katika msimamo wangu wa kusimamia maslahi ya umma...kuna watumishi wachache niliwagusa kidogo baadaye nikaanza kupokea simu toka sehemu mbalimbali...sitishiki wala sitoteteleka"amesema Katwale.
"Tujenge nidhamu ya uwajibikaji kwa majukumu tuliopewa...tambua unapomnyanyasa maskini wa Chato ukiamini wewe siyo mkazi wa huku tambua na ndugu yako atanyanyaswa huko aliko".
Kadhalika ametumia fursa hiyo,kuwataka madiwani hao kujielekeza kwenye kujadili hoja zenye maslahi ya wananchi badala ya maslahi binafsi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Christian Manunga,amewaonya baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo wanaodaiwa kumiliki vikundi vya ujenzi kuacha haraka, na kwamba kazi hizo zielekezwe kwenye vikundi vya wananchi wa kawaida.
"Hatutaki kusikia vikundi vya watumishi wa halmashauri yetu ndiyo vinakwenda kujenga miradi...hii haikubaliki na nawataka mvivunje haraka...na nimelibaini hilo baada ya vikundi hivyo kuvinyima kazi na wenye navyo wakaanza minong'ono...tena na majina yao ninayo siwezi kuyataja hapa"amesema Manunga.
Mwisho.



Post a Comment