Mkuu wa wilaya ya Chato,Deusdedith Katwale,akizungumza na wananchi wa kijiji cha Nyabilezi na Ng'wabaluhi.
Mthamini wa serikali mkoa wa Geita,Nelson Gelbert,akiwaelimisha wananchi wanaotakiwa kupisha eneo la upanuzi wa uwanja wa ndege Chato.
Mkuu wa wilaya ya Chato,Deusdedith Katwale,akizungumza na wananchi wa kijiji cha Nyabilezi na Ng'wabaluhi.
******************************************
Na Daniel Limbe,Chato
MKUU wa wilaya ya Chato mkoani Geita,Deusdedith Katwale,amewasihi wananchi wanaoishi jirani na uwanja wa ndege wa Chato,kukubali kuachia maeneo yao kwaajili ya upanuzi huku akiwasihi wathamini wa serikali kuzingatia sheria,taratibu na kanuni katika ulipaji wa fidia ya ardhi na maendelezo ya wananchi hao.
Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliowahusisha wananchi wa kijiji cha Nyabilezi Kata ya Bukome na kijiji cha Ng'wabaluhi Kata ya Katende ambao maeneo yao yanatarajiwa kutwaliwa na mamlaka ya viwanja vya ndege nchini (TAA).
Katwale, amesema uwepo wa kiwanja cha ndege Chato unalenga kuinua uchumi wa wananchi wa ukanda wa ziwa ikiwa ni pamoja na kuifungua wilaya ya chato kitaifa na kimataifa.
Hata hivyo ametumia fursa hiyo kuwasihi wathamini wa serikali kuwashirikisha wananchi kila hatua ya zoezi hilo,ili kuondoa malalamiko yasiyo kuwa ya lazima ambayo yanaweza kuharibu mahusiano mazuri ya ujirani mwema.
Pamoja na mambo mengine,pongezi nyingi zimwendee mkuu huyo wa wilaya baada ya kurejesha matumaini mapya ya wananchi hao kutokana na malalamiko ya baadhi ya wananchi hao kudai kutapeliwa fedha zao za kuhamisha makaburi kwenye zoezi la mwaka 2021lilifanyika kwa lengo la kupisha ujenzi wa kambi teule ya JWTZ 665 REGT.
Hatua hiyo ilikuja baada ya Shema Bunzali,kumweleza DC kuwa katika zoezi la awali la uthamini liligubikwa na udanganyifu baada ya kuelezwa kuwa walistahili kulipwa shilingi 200,000 ya kifuta machozi kwa kila kaburi na 500,000 zitatumiwa na serikali kuhamisha makaburi jambo ambalo halikutekelezwa.
"Leo mthaminishaji huyu wa serikali anatuambia eti serikali itatumia laki 5 kuhamisha makaburi na laki 2 tutapewa kama kifuta jasho...zoezi la awali tuliambiwa hivi hivi lakini ukweli tuliambulia 200,000 pekee na ndiyo tulizozifanyia kazi ya kuhamisha...serikali haikuonekana kabisa licha ya kutukata 500,000" amesema Bunzali.
Awali mthamini wa serikali mkoa wa Geita,Nelson Gilbert, amesisitiza kuwa zoezi hilo litazingatia taratibu na kanuni zote kwa kuwashirikisha wananchi kila hatua na kwamba kila mtu atakuwa na haki ya kupinga thamani ya mali zitakazoorodheshwa iwapo ataona siyo sahihi.
Mtendaji wa kijiji cha Nyabilezi, Leah Mgogo,amekiri kuipokea timu ya uthamini wa mali za wananchi wake na kwamba baada ya wananchi kuhiari kuachia maeneo yao,timu hiyo inatarajia kuanza kazi mara moja kwa njia ya ushirikishwaji.
Mwisho.



Post a Comment