MLEMAVU WA AKILI ATELEKEZA MTOTO MCHANGA KWENYE DIMBWI





NA Daniel Limbe,Biharamulo

MTU mmoja anayesadikiwa kuwa na changamoto ya afya ya akili wilayani Biharamulo mkoani Kagera,amemtelelekeza pembezoni mwa dimbwi la maji mtoto mchanga mwenye umri wa mwezi mmoja kisha kutokomea kusikojulikana.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya mtu huyo ambaye hajafahamika jina wala makazi yake rasmi kuonekana kijijini hapo akiwa mwenye kuongea peke yake, kuzurura,kulala kwenye mazingira machafu yasiyofaa kwa binadamu ikiwa ni pamoja na kuvua nguo zake hadharani na kubaki uchi mara kadha.

Mwenyekiti wa kitongozi cha Gwabya, Paulo Kaboja,amethibitisha kutelekezwa kwa kichanga hicho, na kwamba jitihada za kumpata mama huyo zimegonga mwamba kutokana na kutojulikana alikokwenda.

"Ni kweli kabisa tukio hilo limetokea kwenye kitongoji changu...mama huyo ambaye ana matatizo ya akili alionekana tangu mwaka hapa kijijini...alikuwa akilala ovyo mitaani na kula kwake ilikuwa ni kuomba omba baadaye tukashangaa kuona mabadiliko ya kimwili kumbe tayali ana mimba" alisema Kaboja.

"Hivi karibuni nikapata taarifa kuwa kajifungua na akawa akizunguka na mtoto wake mitaani...baadhi ya wasamaria wema wakanifuata na kuniambia mtoto yule anaweza kufa kwa sababu mama yake hamnyonyeshi...nikiwa bado natafuta njia za kumsaidia mara nikasikia kuwa katelekeza mtoto na kuondoka zake" aliongeza Kaboja.

Hata hivyo amesema ana uhakika kuwa mhusika wa mimba hiyo atakuwa ni mwenyeji wa mazingira hayo kwa kuwa mama huyo wakati anafika kijijini hapo hakuwa na ujauzito na kwamba amekaa zaidi ya mwaka mmoja, na kwamba mtoto huyo amekabidhiwa kwa Diwani viti maalumu kata ya Nyakahura,ambaye alikubali kumchukua kwaajili ya uangalizi wa awali.

Akizungumza kwenye kikao cha Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo,Diwani huyo Ziyuni Hussein,amesema mama huyo mwenye ulemavu wa akili alimtelekeza mtoto huyo kando ya dimbwi la maji baada ya kumaliza kufua nguo na kuondoka zake kusikojulikana.

Kutokana na hali hiyo,Diwani wa kata ya Kalenge, Erick Method, akashauri mtoto huyo apelekwe kwenye kituo cha malezi ya watoto yatima cha Kalukuta kilichopo jimbo la Rulenge Ngara chini ya kanisa Katoliki kwaajili ya usalama wa afya,malezi na makuzi yake.

Hata hivyo mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Leo Rushau,akawasihi madiwani wake kuchangia kiasi cha fedha toka posho zao kusaidia mahitaji ya mtoto huyo kabla ya kupelekwa kwenye kituo maalumu cha malezi kwa mtoto huyo.

Tatizo la afya ya akili nchini linazidi kuongezeka kila uchao huku baadhi ya  wana jamii wakifanya vitendo vya unyanyapaa na uzalilishaji kwa kundi hilo ambalo halijapewa umuhimu mkubwa katika kunusuru maisha yao. 

                     Mwisho .

0/Post a Comment/Comments