MTENDAJI CHATO ADAIWA KUINGIA NA PANGA OFSINI

 


Madiwani wakiendelea kusikiliza hoja za kikao cha Baraza lao.
Ofisi kuu ya halmashauri ya wilaya ya Chato
Xxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Na Daniel Limbe,Chato

BARAZA la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Chato mkoani Geita, limesikitishwa na tabia za mtendaji wa kijiji cha Nyarutefye kata ya Buziku kuingia ofisini akiwa na panga kwa lengo la kujihami.

Kitendo hicho ambacho kwa mujibu wa sheria za Tanzania ni kosa la jinai,linatajwa kuwa utaratibu wa kawaida kwa mtendaji huyo kuingia kazini na kutoka akiwa na silaha hiyo baridi.

Diwani wa kata ya Buziku, Salama Mgassa,amelieleza baraza la madiwani wa halmashauri hiyo leo wakati akiwasilisha taarifa za maendeleo ya kata yake,huku akiomba kubadilishiwa mtumishi huyo kutokana na vitendo vinavyotishia amani kwa wananchi.

"Mwenyekiti niliombe Baraza lako lisaidie kupata mtendaji mwingine kutokana na aliyepo kwenye kijiji cha Nyarutefye kuingia ofsini kwake akiwa na panga ambalo hudai ni kwaajili ya kujihami" amesema Mgassa. 

Kauli hiyo mbali na kuibua mshituko mkubwa kwa madiwani hao,wamesema ipo haja kubwa kwa serikali kumuondoa mtendaji huyo kwenye kituo hicho na kupangiwa sehemu nyingine wakati mwajili wake akiwa anatafuta namna ya kumwajibisha.

Makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Photunatus Jangole, akamwagiza Ofisa utumishi kumwajibisha mtendaji huyo ikiwa ni pamoja na kumripoti kituo cha polisi ili awajibishwe kwa kutenda kosa la jinai.

Akitoa ufafanuzi kwa niaba ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo,Ofisa utumishi, Martine Ndamo, ameahidi kuwasilisha taarifa hizo kwa jeshi la polisi ili hatua zingine zifuate huku akidai kwa sasa halmashauri hiyo ina uhaba mkubwa wa watendaji  jambo linalosababisha baadhi ya vijiji kutokuwa na watendaji.

Mbali na hilo, Diwani wa kata ya Bwanga,James Kahola, amedai kituo cha afya Bwanga wanalazimika kutumia tochi kutibu wangojwa baada ya umeme kukatika huku wakiomba kupewa jenereta.

"Mwenyekiti kwenye kata yangu tuna changamoto ya ukosefu wa Jenereta...umeme wa Tanesco unapokatika watumishi wanalazimika kutumia tochi kutibu wagonjwa na wengine wanatoroka wodini pasipo kulipa gharama za matibabu" alisema Diwani Kahola.

Kikao cha Baraza la madiwani Chato kimefanyika leo kwa kila diwani kuwasilisha taarifa za maendeleo ya kata yake huku changamoto kubwa ikiwa ni ukusanyaji mapato ya halmashauri hiyo.

                   Mwisho.

0/Post a Comment/Comments