Xxxxxx xxxxxxxxxx xxxx x
Na Daniel Limbe, Biharamulo
WATU watatu wa familia moja akiwemo mjamzito wamepoteza maisha baada ya kupigwa na radi wilayani Biharamulo mkoni Kagera huku wengine watatu wakijeruhiwa na kupelekwa hospitali.
Tukio hilo ambalo limetokea juzi januari 29 mwaka huu kwenye kijiji cha cha Kiruruma kata ya Bisibo wilayani hapa liliwakumba watu sita wa familia moja huku Baba wa familia hiyo akinusurika baada ya kuegama mvua mbali na (mkamwana) mke wa mwanaye wa kiume.
Akizungumza Torch Media Diwani wa Kata ya Bisibo,Festo Mtatembwa,amesema wananchi hao walikumbwa na umauti huo wakati wameegama mvua chini ya mti baada ya kunyesha wakati wakipanda mpunga shambani kwenye eneo la Nyarwambu kitongoji cha Nyabiondo.
Aliwataja waliopoteza maisha kuwa ni mama wa familia, Ester Nyanda, Elisha Mstapha( mtoto) na Semen Seleman(mkamwana ambaye ni mjamzito).
Waliojeruhiwa ni Fabian Mstapha( mtoto), Jenipha Mstapha(mtoto) na Frenk Mstapha( mtoto) huku Baba wa familia hiyo Tusabe Mahame akibaki salama kati ya watu saba waliokuwa shambani hapo.
Mtatembwa amesema baada ya mvua hiyo kuanza kunyesha baba wa familia hiyo, aliondoka eneo hilo na kwenda kuegama sehemu nyingine, kutokana na imani za jamii hiyo kutokaribiana na mka mwana wake(mke wa mtoto wake) jambo ambalo lilimsaidia kunusurika na majeruhi au kifo.
Mwenyekiti wa kijiji cha Nyakiruruma,Elizeus Nestory, amekiri kutokea kwa vifo na majeruhi hao na kwamba baada ya kulijulisha jeshi la polisi wilayani Biharamulo,jana februali 30 walifika eneo la tukio na kuwaruhusu wananchi kuendelea na mazishi baada ya kukamilisha taratibu zao.
Aidha amesema tukio hilo ni la kwanza kitokea kwenye kijiji hicho na kwamba limezua simanzi kubwa kwa wakazi wake licha ya kuwasihi kulipokea kama tukio la kawaida kwenye jamii badala ya kulihusisha na imani za kishirikina.
Mganga mkuu wa hospitali teule ya wilaya ya Biharamulo,Grasimus Sebuyoya,amekiri kupokea majeruhi watatu na kwamba wameruhusiwa kuondoka baada ya hali zao kuimalika.
Kamanda wa polisi mkoani Kagera,William Mwampaghale, hakupatikana kutokana na simu yake kuita bila kupokelewa na jitihada za kumtafuta zinaendelea.

Post a Comment