Kamanda wa polisi mkoa wa Geita,Safia Shomary, akiwa na viongozi mbalimbali wilayani Chato leo.
Jeshi la akiba (mgambo) wakiwa pembezoni mwa mkutano huo wakimsikiliza kamanda wa polisi mkoa wa Geita.Na Daniel Limbe,Chato
KAMANDA wa polisi mkoa wa geita, Safia Shomary, amewaonya askari polisi walevi na wale wapya waliotoka vyuo vya polisi kuacha kuwanyanyasa wananchi badala yake wazingatie maadili na miongozo ya jeshi hilo.
Ameyasema hayo leo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya stendi ya zamani ya mabasi ya chato mjini,ambapo amelazimika kutoa onyo hilo baada ya wananchi kulalamikia unyanyasaji huo.
Awali Alex Mkama,mkazi wa chato mjini alionekana kulinyooshea kidole jeshi hilo kutokana na vitendo vya unyanyasaji unaofanywa na baadhi ya polisi vijana waliotoka vyuoni.
Ameyataja baadhi ya manyanyaso hayo kuwa ni kuwapiga vilungu sehemu mbalimbali za miili yao wananchi ambao baadhi yao hukamatwa majumbani mwao pasipo kuelezwa makosa yao na wengine kubambikiwa kesi za uzurulaji kinyume cha sheria.
Kadhalika amedai baadhi ya askari hao ni walevi kupindukia na kwamba baadhi yao nyuso zao zimejaa ngeo ikidhihilisha wazi kuwa ni wakolofi.
Hata hivyo Mkama amegusia udhaifu wa dawati la jinsia kwa jeshi la polisi wilayani chato,na kwamba vitendo vya unyanyasaji kijinsia kwa wanaume umekuwa ukitamalaki kila uchao lakini hawapewi kipaumbele cha kushughulikia matatizo yao ukilinganisha na wanawake.
Anasema hali hiyo imesababisha baadhi ya wanaume kuzikimbia familia zao na wengine kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani baada ya kuwajeruhi wenza wao na kutokomea kusikojulikana
Kutokana na hali hiyo, Kamanda Shomary, akatumia fursa hiyo kuwaonya askari wake huku akiwatala kuacha vitendo vya ulevi na unyanyasaji wa raia na kwamba hata mwonea huruma askari yoyote atakaye kiuka sheria,taratibu na kanuni za jeshi hilo.
Hata hivyo ameagiza kuimalishwa dawati la jinsia wilayani humo ili wanaume nao wahudumiwe kikamilifu kama ilivyo kwa wanawake,sambamba na kuwataka wanawake kukejea kwenye mila na desturi za kitanzania kwa kuheshimu na kutii waume zao ili kudumisha ndoa zao.
Diwani kata ya Chato,Mange Ludomya,mbali na kumpongeza kamanda huyo wa polisi kwa kuanzisha utaratibu mpya wa kuitisha mikutano ya hadhara kusikiliza kero za wananchi,amemtaka kuendeleza mahusiano hayo ili kutoa mwanya kwa wananchi kushirikiana na jeshi hilo ikiwemo kuwasilisha taarifa za siri za uharifu na waharifu.
Mkutano huo wa hadhara ni wa kwanza kwa kamanda wa polisi mkoa wa geita tangu alipowasili mkoani hapa.


Post a Comment