TANZANIA NA BENKI YA DUNIA ZASAINI MKOPO NAFUU TRIL1.264

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Nathan Belete wakisaini Mikataba miwili ya mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 550 (sh. trilioni 1.264) na msaada wa dola za Marekani milioni 29.93 (shilingi bilioni 68.51) kwa ajili ya kuboresha sekta za maji na usafi wa mazingira mijini na vijijini na mradi wa kuboresha afya ya mama na mtoto.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bw. Nathan Belete wakionesha Hati za Mikataba miwili ya mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 550 (sh. trilioni 1.264) na msaada wa dola za Marekani milioni 29.93 (shilingi bilioni 68.51) kwa ajili ya kuboresha sekta za maji na usafi wa mazingira mijini na vijijini na mradi wa kuboresha afya ya mama na mtoto Tanzania Bara na Zanzibar



Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (Katikati), Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bw. Nathan Belete (Wapili kushoto), Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Godwin Mollel (Watatu kulia), Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Natu Mwamba, wa pili kulia na  Naibu Wake Amina Khamisi Shaaban, pamoja na Mkurugenzi Mkuu-Wizara ya Afya Zanzibar Dkt. Amour Mohamed (kushoto) mstari wa mbele, wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Tanzania na Benki ya Dunia

.............................

NA MUSSA KHALID

Serikali ya Tanzania  na Benki ya Dunia zimesaini mikataba miwili ya  masharti nafuu kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Afya ya Mama na Mtoto pamoja na Mpango Endelevu wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini yenye thamani zaidi ya shilingi trilioni 1.264 pamoja na misaada ya shilingili bilioni 68.79 kwa ajili ya utekelezaji miradi hiyo.

Hayo yamejiri Leo jijini Dar es salaam katika hafla ya utiaji saini miradi miwili muhimu ya maendeleo chini ya mzunguko wa IDA-20 wa Benki ya Dunia ukiwemo miradi mpango endelevu wa huduma ya maji na Afya ya mama na watoto Tanzania baina na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Mwigulu Nchemba na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Tanzania  Nathan Belete.

Akizungumza katika hafla hiyo  Waziri wa fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kwa kusaini mikataba hiyo, Benki ya Dunia imeongeza kiwango cha jumla ya fedha zilizotolewa kama mkopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo hapa nchini kwa ya kitaifa na kikanda kufikia dola za Marekani bilioni 7.8.

Aidha amesema kuwa Benki ya Dunia imeendelea kuwa mshirika mkubwa na wa kutegemewa wa Tanzania kwa ufadhili wake mkubwa katika miradi ya maendeleo hivyo Watanzania wanathamini na wataendelea kuthamini ushirikiano wao wa maendeleo.

"hafla hii ya utiaji saini ni ishara ya mwendelezo wa ushirikiano mkubwa baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Dunia kwa miongo kadhaa, ambapo idadi kubwa ya miradi inayolenga kupunguza umaskini, kuongeza ustawi wa pamoja na kukuza maendeleo endelevu kwa watanzania imetekelezwa. Hakika tunajivunia ushirikiano huu na tutaendelea kuimarisha ushirikiano wetu kwa manufaa ya pande zote na kwa Taifa kwa ujumla"amesema Dkt Nchemba

Awali wakizungumza Naibu Waziri wa Afya Tanzania Dkt Godwin Mollel amesema kuwa Fedha walizozipata zitakwenda kuwezesha huduma ya mama na Mtoto lakini pia wataweza katika kujenga vituo vya watoto njiti.

Amesema, Dola za Marekani milioni 244 zilitolewa na Banki kuu ya Dunia kupitia mpango harakishi wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 556 katika vizazi hai 100,000 (TDHS 2015) mpaka vifo 238 katika vizazi hai 100,000 (WHO 2023).

Aidha, Dkt. Mollel ameeleza vifo vya watoto vimepungua kutoka 67 katika vizazi hai 1,000 (TDHS 2021) mpaka 43 katika vizazi hai 1,000 (TDHS 2022) sawa na asilimia 35%, ingawa hali hiyo haifanani kwenye kwa vifo vya watoto wachanga wanaozaliwa, ambayo inaonesha kushuka kutoka vifo 25 kwa vizazi hai 1,000  (TDHS 2015) mpaka vifo 24 katika vizazi hai 1,000 (TDHS 2022).

Naye Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dkt Amour Suleiman Mohammed akiipongeza Benki ya Dunia lwa kuonyesha mashirikiano kwa Muda mrefu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Tanzania Nathan Belete amesema miradi hiyo miwili ni muhimu kwa ajili ya kutatua changamoto zinazowakumba watanzania ikiwemo katika sekta ya afya pamoja na mpango endelevu wa maji na usafi wa mazingira vijijini.

Dkt Nchemba amesema kuwa serikali imejizatiti kuhakikisha inafanikiwa kufikia ukuaji wenye stahilimivu, jumuishi, uthabiti na endelevu kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Benki ya Dunia na kufikia malengo.

0/Post a Comment/Comments