Baadhi ya wakulima wa kijiji cha Kashanda wakiwa kwenye ujenzi wa chumba cha darasa la watoto wa shule ya awali.
Baadhi ya mashamba ya migomba na mibuni ambayo yanamilikiwa na wakulima kwenye kijiji cha Kashanda wilayani Karagwe.
Na Daniel Limbe,Karagwe
WAKULIMA na wafugaji waliohasimiana kwa zaidi ya miaka 30 kwenye kijiji cha Kashanda wilayani Karagwe mkoani Kagera,wameweka tofauti zao kando na kuanza ujenzi wa chumba cha darasa la shule ya awali ili kupunguza adha ya watoto wao kutembea umbali mrefu.
Awali makundi hayo yamekuwa na msigano wa kugombea ardhi muda mrefu na kusababisha kudumaa kwa maendeleo ya kijiji hicho,huku zaidi ya wakulima sita wakiuawa mwaka 2015 pamoja na ng'ombe 117 kukatwa mapanga.
Kutokana na hali hiyo, pongezi nyingi zinaelekezwa kwenye mazungumzo na mpango bora wa matumizi ya ardhi,uliosaidia kumaliza changamoto hiyo, hatimaye wananchi hao kuanza kuchangia maendeleo yao kwa kuipa kipaumbele elimu ,kutokana na wanafunzi kulazimika kutembea umbali mrefu kati ya km 10 hadi 12 kuifikia shule ya msingi Omrusimbi.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi, Omrusimbi,Simon Rumanyika, ameiambia Torch media kuwa jamii ya wakulima na wafugaji wa kijiji hicho wamechangishana fedha,nguvu na vifaa vya ujenzi kisha kujenga darasa moja la watoto wanaopaswa kusoma shule ya awali pasipo kutembea umbali mrefu ambao umekuwa ikisababisha watoto wengi kutohudhuria masomo.
Baadhi ya wakulima hao, Sudy Kabyemela na Abdon James, wamesema mafanikio hayo yanatokana na kumalizika kwa mgogoro mkubwa kati ya wakulima na wafugaji ambao awali ulisababisha baadhi ya wakulima kuyakimbia makazi yao kutokana na mauji ya mara kwa mara.
"Kwa kweli tunaipongeza sana serikali kwa kuunga mkono jitihada zetu za kumaliza mgogoro wa ardhi ambao ulisababisha vifo vya watu na mifugo...tulikuwa hatuwezi kukaa pamoja wala kusalimiana ila mpango wa matumizi bora ya ardhi umetusaidia kuwa pamoja na sasa tumeanza ujenzi wa darasa la watoto wa shule ya awali kwa nguvu na michanho yetu" wamesema.
Kwa upande wao baadhi ya wafugaji wa kijiji cha Kashanda, Chifu Millard Silvester na Edward Chiza, wanakiri kuwa awali hali ya mahusiano ya kijamii ilikuwa mbaya sana na kwamba baadhi ya watu walipoteza maisha pamoja na baadhi ya mifugo yao kuuawa na wakulima chanzo kikiwa ni kugombea ardhi kwaajili ya kilimo na malisho ya wanyama (Ng'ombe).
"Sasa hivi tunaishi kwa amani hatuna tena ugomvi...kila upande unaheshimu eneo la upande mwingine na hii imesababishwa na uwepo wa matumizi bora ya ardhi...japo kuna baadhi ya wanasiasa ambao hawakufurahishwa na uamuzi huu kutokana na maslahi waliokuwa wakiyapata kutokana na ugomvi wetu" amesema Chifu Silvester.
Ofisa Kilimo na mifugo wilaya ya Karagwe,Adam Salum, amesema hivi sasa hali ni shwari hakuna tena mapigano yoyote kwa jamii hiyo kutokana na uwepo wa mpango wa matumizi bora ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji kwenye kijiji hicho.
Polisi mlezi wa Kata ya Nyakahanga, A/ INSP. Adam Kiwori,amethibisha kuwepo kwa amani kubwa kwenye kata hiyo na kwamba mauaji ya watu na mifugo yalikuwepo kipindi cha nyuma ikilinganisha na sasa ambapo makundi yaliyokuwa yakihasimiana sasa wanaishi pamoja.
Wakili Raymond Laurent,kutoka shirika la msaada wa kisheria la MHOLA lililopo wilayani humo mkoani Kagera,amesema uwepo wa migogoro katika jamii hufubaza maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla na kwamba ipo haja kubwa ya migogoro ya ardhi kumalizwa kwa njia ya usuluhishi ili kujenga amani na maelewano mema kwa pande hasimu.
Mwisho.




Post a Comment