CRDB YATOA KAULI NZITO UPOTOSHWAJI TAWI LA CHATO

 

Huduma za kifedha zikiendelea kutolewa ndani ya CRDB tawi la Chato.
Mwonekano wa nje wa Benki ya CRDB Chato
Mmoja wa wateja akitoka ndani ya Benki hiyo baada ya kupata huduma.

***************

Daniel Limbe,Chato

SIKU chache baada ya kuibuka uvumi kwenye baadhi ya vyombo vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii kuwa Benki ya CRDB tawi la Chato imefungwa na kugeuka klabu ya usiku (ukumbi wa muziki) hatimaye uongozi umeibuka na kutoa kauli nzito.

Uvumi huo umezua taharuki kwa baadhi ya watu baada ya kutumainishwa uongo wenye lengo la kuchafua taswira pana ya huduma bora za benki hiyo jambo ambalo linadaiwa siyo la kufumbia macho.

Wakiwa na lengo ovu kwa benki ya CRDB na jamii kwa ujumla,walidai kuwa tawi hilo lilifungwa siku chache baadaa ya kifo cha aliyekuwa rais Tanzania,Hayati Dk. John Pombe Magufuli,ambaye alikuwa ni mzaliwa wa mji wa Chato mkoani Geita,huku baadhi yao wakidai alitumia nguvu za kiutawala kujengwa benki hiyo licha ya kutokuwapo wateja.

Pamoja na propaganda nyingi za uongo,bado watu hao walipotosha kuwa uwanja wa ndege Chato haufanyi kazi tena,stendi ya mabasi ya "Kahumo bus terminal" nayo imetelekezwa na kubaki magofu jambo ambalo siyo kweli.

Kutokana na hali hiyo, Meneja wa CRDB tawi la Chato,Daniel Nyamivugwa,amekanusha vikali uvumi huo na kudai kwamba uongozi wa benki hiyo makao makuu unakusudia kuchukua hatua kali kwa wote waliohusika kuchafua taswira nzuri ya benki hiyo kwa malengo yao binafsi.

"Benki yetu ipo imara na inaendelea kutoa huduma siku zote kama leseni yetu inavyotaka...wananchi wasiwe na wasiwasi na uongo unaoenezwa...waje tuwahudumie ili waweze kujikwamua kiuchumi".

"Wilaya ya Chato inaendelea kukua kutokana na baadhi ya watu kuendelea kuwekeza kwenye viwanda,migodi na biashara...hata hivyo kundi la wakulima tumelipa kipaumbele sana kwa kuwapatia mikopo yenye riba nafuu ya aslimia 9 pekee...hii nikutokana na ukweli kwamba aslimia kubwa ya wakazi wanajishughulisha na kilimo,ufugaji na uvuvi"amesema Nyamivugwa.

Pia Benki hiyo imeahidi kushirikiana na serikali ya wilaya hiyo katika mpango mkakati wa kilimo cha umwagiliaji kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa chakula na kuinua uchumi wa jamii na taifa kwa ujumla.

Mmoja wa wafanyabiashara wilayani hapa,Timotheo Maize,anasema kilichozungumzwa kwenye mitandao ya kijamii ni upuuzi mtupu kutokana na kile anachosema kuwa yeye ni mteja wa CRDB na anaendelea kunufaika na mikopo ya biashara.

Mkuu wa wilaya ya Chato, Deusdedith Katwale,amewataka wananchi kupuuza uongo huo na kwamba wilaya hiyo inaendelea kusonga mbele ki maendeleo na kwamba hakuna mradi hata mmoja ulioanzishwa na serikali ya awamu ya tano utakao kwama kukamilika.

"Mara kadhaa rais wetu Samia Suluhu Hassan ameendelea kusema kuwa miradi yote aliyoianzisha Hayati Dk. Magufuli kwenye wilaya yetu itakamilika...lakini baadhi ya watu wenye nia mbaya na wilaya yetu wamekuwa wakipotosha jamii kuwa tangu kifo cha Hayati Magufuli mambo yamesimama".amesema Katwale.

"Ni wahakikishie kuwa rais Samia bado ana nia njema sana na wilaya yetu...ndiyo maana pesa nyingi ya maendeleo zinakuja na sisi wasaidizi wake tunaendelea kufuatilia kuhakikisha fedha zote zinakwenda kwenye miradi iliyokusudiwa na inatekelezwa.kwa viwango vinayokubalika".

Ikiwa imetimia miaka miwili tangu kufariki kwa aliyekuwa rais wa Tanzania, Hayati Dk.Magufuli,jamii inaendelea kumkumbuka kwa mchango wake mkubwa kwa taifa letu ikiwa ni pamoja na Tanzania kuifikisha kwenye nchi zenye uchumi wa kati,huku rais Samia Suluhu Hassan, naye akiendeleza vyema kijiti alichoachiwa na mtangulizi wake.

                        Mwisho.

0/Post a Comment/Comments